Header Ads Widget

ANAYETUHUMIWA KUKEKETA WATOTO AFIKISHWA MAHAKAMANI




Mtuhumiwa wa kesi za ukatili dhidi ya watoto (ukeketaji), Mugesi Mogoyo (katika) akiwasili katika viunga vya Mahakama ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara chini ya ulinzi wa Polisi waliomzunguka, ambapo kesi hizo ziliahirishwa baada ya mtuhumiwa kukana mashitaka na kuahirishwa mpaka zitakaposikilizwa tena mahakamani hapo.
MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Mugesi Mwita Mogoyo (50) mkazi wa Kitongoji cha Nyahende Kijiji Cha Kitarungu wilayani Serengeti mkoani Mara, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Serengeti mkoani Mara akikabiliwa na makosa mawili ya ukatili dhidi ya watoto (ukeketaji) aliyoyatenda kwa nyakati mbili tofauti kinyume cha sheria.

Akisoma shitaka la kwanza la kesi namba 170 ya mwaka 2020 iliyosikilizwa na Hakimu Adelina Mdhalifu, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Paschal Nkenyenge aliiambia mahakama kuwa, mtuhumiwa alitenda kosa hilo April 13, mwaka huu Kijiji cha Kitarungu majira ya usiku kinyume cha kifungu cha Sheria namba 169 A (1) ( 2) cha kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya mwaka 2019.

Mara baada ya mtuhumiwa kusomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu Mdhalifu, mtuhumiwa alikana na kusema kuwa yeye hakufanya kosa hilo na ndipo hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Adelina Mdhalifu, alipoihairisha mpaka Juni 22, mwaka huu itakaposikikizwa tena mahakamani hapo.

Aidha, katika kosa la pili la kesi namba 157 ya mwaka 2020 inayomkabili Mugesi Mugoyo iliyosikilizwa na Hakimu Judith Semkiwa, Mwendesha Mashitaka upande wa Serikali wa kesi hiyo (PP) Faru Mayengela, aliimbia mahakama hiyo kuwa, mtuhumiwa huyo Mugesi Mwita alitenda kosa la ukatili dhidi ya mtoto Kijiji Cha Kitarungu mnamo Aprili, 11 mwaka huu majira ya usiku, huku akijua ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mara baada ya kusomewa shitaka linalomkabili na mwendesha ashitaka upande wa Serikali (PP) Faru Mayengela mtuhumiwa huyo alikana kosa mbele ya Hakimu Semkiwa.

Baada ya mtuhumiwa kukana kosa hilo, Hakimu aliyekuwa akisikiliza shauri hilo Judith Semkiwa, aliiahirisha kesi hiyo mpaka itakaposikikizwa tena mahakamani hapo Juni 22, mwaka huu na mtuhumiwa amerejeshwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini.
CHANZO-MAJIRA