Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
Askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoa wa Shinyanga, Idiphonce Sadick Nyamburi (32) mwenye namba G4793 PC amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akitembea barabarani.
Ajali hiyo ilitokea jana Juni 10, 2020 saa 9:30 alasiri katika barabara ya Dami hoteli eneo la mjini kati katika manispaa ya Shinyanga, ambapo marehemu Iddi akiwa anatembea barabarani na mwenzake Ngassa Mabula (27) waligongwa na gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 788 DFW mali ya Nobert Masanja lililokuwa likiendeshwa na Paul John (38) mkazi wa Buzuka mjini humo.
Akisimulia tukio hilo, Ofisa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi Audax Majaliwa amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe ambapo dereva huyo aliwagonga watembea kwa miguu wawili akiwemo askari huyo ambaye aliumia vibaya kichwani na kuvunjika mguu wa kulia na akafariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Majaliwa ambaye ni Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, alisema mhanga mwingine wa ajali hiyo aliyetambulika kwa jina la Ngassa Mabula (27) mkazi wa kata ya Ndala mjini Shinyanga alipata majeraha madogo na alitibiwa na kuruhusiwa.
"Ajali hii ilitokea Juni 10, 2020 saa 9:30 Alasiri eneo la Mjini Kati
barabara ya Dami Hoteli, ambapo gari hilo likiendeshwa na Paul John aligonga watembea kwa miguu wawili akiwemo askari wetu namba G4793PC
wa kikosi cha FFU mkoa wa shinyanga aliumia vibaya
kichwani na kuvunjika mguu wa kulia na kusababisha kifo chake wakati akipatiwa
matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
"Majeruhi mwingine (Ngassa Mabula) alipata
majeraha madogo na alitibiwa na kuruhusiwa. Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea, lakini dereva na
gari lililosababisha kifo hicho tayari viko mikononi mwa polisi na uchunguzi
ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa," amesema Majaliwa.
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Majaliwa aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa makini na
utunzaji wa funguo za magari pale wanapokuwa wanahifadhi, na waangalie nani
anatumia gari na ana utaalamu wa kiasi gani na kama hana leseni inakuwa ni
tatizo.
"Ukiangalia tukio hilo limetokea kwa uzembe na mzembe lazima
achukuliwe hatua za kisheria," amesema.