Balozi Ali Karume amechukua fomu kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia ameahidi kuimarisha muungano kwa manufaa ya Wanzania wa pande zote mbili za Muungano huo.
“Iwapo nitateuliwa, nategemea kuendeleza dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kulinda muungano wetu na kuendeleza Sera ya CCM, Dk. Ally Shein, rais wangu amefanya kazi ya kupigiwa mfano hasa kuendeleza sera zilizoanzishwa na Abeid Karume, nia yangu ni kuendeleza yote mazuri,” amesema Karume.
Karume ambaye kwa sasa ni Waziri wa Vijana Utamaduni, Michezo visiwani Zanzibar, amesema endapo atapata nafasi ya kuwa rais wa nchi hiyo, ataboresha utolewaji wa huduma za kijamii, ikiwemo afya, elimu makazi ya watu, ugawaji wa ardhi kwa wananchi wote.
“Nitahakikisha afya inaendelea kupatikana bila malipo, elimu ipatikane bila malipo, ugawaji ardhi uendelee kwa wananchi wanaohitaji kwa masuala ya kilimo na ujenzi. Nitajenga makazi bora, Mzee Shein amejenga nyumba nzuri lakini nimeona zinahitaji ukarabati, hilo naahidi tutalifanya pamoja na mengineyo,” amesema Karume