POLISI wilayani Bunda Mkoa wa Mara inamsaka Magige Igone, kwa madai
ya kumbaka binti yake ambaye pia ni mwanafunzi wa darasa la saba katika
Shule ya Msingi Miembeni B iliyoko Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyamuswa, Simon Joseph, akisimulia tukio
hilo juzi mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, aliyekuwa
na wajumbe wa kamati ya maadili ya mahakama katika wilaya hiyo, alidai
kuwa Igone alimbaka mtoto wake hivi karibuni nyumbani kwake katika
Kijiji cha Nyamuswa majira ya usiku.
Kwa upande wake, mtoto huyo akisimulia tukio hilo alidai kuwa baba
yake alianza kumtongoza akisema atampatia Sh 5,000 na alipomkatalia
ndipo usiku alipomvamia ndani ya chumba chake na kumkamata kwa nguvu
huku akiwa amemziba mdomo kwa mikono yake.
Alidai kuwa siku hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa baba yake kumfanyia
ukatili huo na kwamba baada ya kufanyiwa kitendo hicho alikimbia na
kupiga yowe, na shangazi yake alifika kumchukua na akamlazimisha kuoga
ili asionekane kama amebakwa.
“Hii ni mara ya pili baba ananibaka, siku ya kwanza alinifanyia hivyo
akaniambia kama nikisema sehemu yoyote ataniua. Sasa ile siku ya pili
aliniambia anipe Sh 5,000 tulale naye, nikakataa ndipo usiku akanigongea
mlango eti akiomba maji ya kunywa.
“Mimi nikamwambia ‘baba si maji unayo huko’ akanilazimisha ndipo
nikafungua na kumpatia maji, nilivyotaka kufunga mlango akaweka mkono
wake nikashindwa kuufunga, ndipo aliponivamia kwa nguvu na kunifanya
kitendo hicho,” alidai mwanafunzi huyo.
Kwa upande wao polisi walisema shangazi ya binti huyo alikamatwa na kwamba wanaendelea kumsaka baba yake ambaye alitoroka.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bupilipili, alilitaka Jeshi la Polisi
wilayani hapa kumsaka mwanaume huyo ili afikishwe kwenye vyombo sharia
kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464