Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwa amenyanyua mkoba wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2020/2021 Bungeni jijini Dodoma.
Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
NI bajeti ya kumjali Mtanzania na kuleta maendeleo kwa Watanzania wote.Hivyo ndivyo unavyoweza kuieleza Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021 yenye jumla ya Sh.trilioni 34.88 .
Bajeti hiyo ambayo imewasilishwa leo Juni 11,2020 Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango ndio ya mwisho katika mhula wa kwanza wa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli.
Wakati inasomwa bajeti hiyo na Waziri Dk.Mpango kwa sehemu kubwa imeonesha kuwa ni bajeti yenye unafuu kwa makundi yote katika jamii ya Watanzania yakiwemo ya wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wafanyabiashara pamoja na wajasiriamali.
Pamoja na mambo mengine bajeti hiyo Waziri Mpango ameeleza namna ambavyo yamefanyika marekebisho ya kikodi yanayolenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na hasa kwenye sekta ya kilimo pamoja na viwanda.Dk.Mpango amefafanua pia jumla ya tozo na ada 114 zimefutwa katika mapendekezo ya marekebisho yanayopendekezwa kwenye maeneo 16.
Akifafanua zaidi wakati akiwasilisha bajeti hiyo mbele ya Wabunge ,Dk.Mpango amesema katikakuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, sura ya bajeti inaonesha kuwa jumla ya sh. trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.
Amefafanua kwamba jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 24.07, sawa na asilimia 69.0 ya bajeti yote na kwamba kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya Sh.trilioni 20.33, mapato yasiyo ya kodi ya Sh.trilioni 2.92 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri Sh. bilioni 815.0.
Pia amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia bajeti hiyo inatarajia kukopa Sh. trilioni 4.90 kutoka soko la ndani na kati ya kiasi hicho cha fedha Sh.trilioni 3.32 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva huku Sh.trilioni 1.59 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
"Shilingi trilioni 3.04 zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.Washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya sh. trilioni 2.87 ambayo ni asilimia 8.2 ya bajeti. Kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo ni Sh. trilioni 2.46, Mifuko ya Pamoja ya Kisekta Sh.bilioni 138.3 wakati misaada na mikopo ambayo nafuu ya kibajeti ni Sh. bilioni 275.5,"amefafanua.
Pamoja na mambo mengine mengi ambayo Waziri Mpango ameeleza katika bajeti hiyo ametumia nafasi hiyo kueleza kwa upande wa tozo zilizokuwa zikitozwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, amependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427 kwa kupunguza ada na tozo zifuatazo.
Dk.Mpango amezitaja tozo hizo ni kupunguza tozo ya Cheti cha Umahiri inayotozwa kwa wauzaji wa vifaa vya zimamoto na uokoaji kutoka sh. 500,000 hadi sh. 200,000.Pia kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa usiozidi mita za mraba 2,000 kutoka sh. milioni 6,000,000 hadi sh. 100,000.
Waziri Mpango amesema kuwa amependekeza kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 2001 hadi 4000 kutoka sh. milioni 6,000,000 hadi sh. 150,000.Pia kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya 110 uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 4001 hadi 9000 kutoka sh. milioni sita hadi sh. 200,000.
Kwa mujibu wa Waziri huyo ni kwamba wamepuguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 1 hadi tani 10 kutoka sh. milioni mbili hadi sh. milioni 1.5. Aidha, kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maduka yanayouza mitungi ya gesi yasiyozidi ukubwa wa mita za mraba 100 kutoka sh. 100,000 hadi sh. 40,000.
Mbali na hayo katika bajeti hiyo amependekeza kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maduka ya rejareja na maduka ya jumla kutoka sh. 40,000 hadi sh. 20,000, kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye vituo vidogo 111 vya kuzalisha na kugawa umeme chini ya Megawati 10 kutoka sh. milioni sita hadi sh. 200,000.
Pia amependekeza kufanya kwa marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427, ili kuanzisha viwango vipya vya tozo kama ifuatavyo, kutoza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto ya sh. milioni mbili kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 11 hadi tani 20.