Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Alli Idd akizungumza Jana mjini Kahama.
Salvatory Ntandu - Kahama
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Balozi Seif Alli Idd amewataka viongozi wa ngazi za matawi, kata, wilaya na Mikoa kuzipokea fedha zinazotolewa na baadhi ya watia nia wanaotaka uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani shinyanga na kuwafichua kwa vyombo vya usalama ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Kauli hiyo ameitoa Juni 26, mwaka huu wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo akiwa ni mlezi wa CCM wa mkoa huo baada ya kupokea taarifa ya chama kuhusiana na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020.
Alisema kuwa kiongozi anayenunua kura hafai kuwemo ndani ya CCM mpya inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Maguli kwani atatanguliza mbele Maslahi yake binafsi pindi atakapochaguliwa.
"Wapo wapambe wa wagombea wameanza kuunguka katika matawi na kata na kugawa Sh 5,000 hadi e20,000 zipokeeni lakini msiwachague kwa sababu CCM inautaratibu wake wa kuwapata viongozi," alisema Balozi Idd
Aliongeza kuwa CCM haitapitisha jina la mgombea yeyote atakayebainika kutoa fedha ili kupata nafasi ya kuchaguliwa hata kama atakuwa amepitishwa na mikutano mikuu ndani ya chama ili kutokomeza vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi.
"Vyombo vyetu vya dola vimejipanga kikamifu kudhibiti vitendo vya rushwa ambavyo husababisha wagombea wasiokuwa na sifa kuchaguliwa ambao sio chaguo la wananchi na kuwakosesha watu wenye sifa kuchaguliwa," alisema Balozi Idd.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Gaspar Kileo ambae pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa (NEC) aliwataka makatibu wa matawi, kata na wilaya kuwachukulia hatua kali watia nia ambao watakaobainika kuanza kampeni kabla ya muda wao.
"Wakamateni ili vyombo vyetu viwafanyie kazi kwa kutoa rushwa halafu wakija kwenye chama sisi hatutapitisha majina yao," alisema Kileo.
Kuanzia Julai 7 hadi 14 mchakato wa uchukuaji wa fomu ndani ya CCM utaanzaa ambapo kwa sasa watu wote wanaotaka kugombea nafasi za ubunge na udiwani kutoruhusiwa kufanya kampeni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Alli Idd akipokelewa na baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM mkoa wa Shinyanga alipowasili kwa ziara ya siku kadhaa mkoani humo.