CHADEMA: HATUTASUSIA UCHAGUZI MKUU 2020


Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, Benson Kigaila akisisitiza  umuhimu wa chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu ambao unatarajia kufanyika mwezi Oktoba.

Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimebainisha kuwa hakitajitoa katika uchaguzi   mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huuu kama kilivyofanya katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba, mwaka jana pale chama hicho kilipoamua kujitoa kushiriki kwa madai ya uchaguzi huo kuvurugwa na kutawaliwa na rafu.

Hayo yameelezwa jana Juni 21, 2020 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, Benson Kigaila wakati akizungumza na watia nia kutoka Majimbo yote ya Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu, katika makao makuu ya Kanda hiyo yaliyopo Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Kigaila ameeleza kuwa tangu chama hicho kiundwe hakijawahi kuomba huruma kutoka kwa watawala ambapo mwaka 1995 walipata madiani 15  na wabunge wanne, huku katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wakifanikiwa kupata wabunge 73 na madiwani  1108, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanashindana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 “Ujumbe huu uwafikie, uchaguzi huu tunaenda kushiriki hakuna wa kujitoa, tunakwenda tukijua hakuna tume huru, wanatunga sharia zozote wanazotaka tumeamua kusiwe na tume huru, uchaguzi tunakwenda kushinda na kutangazwa kituoni kwa ushindi,” alisema.

Katika hatua nyingine Kigaila amewataka wanachama kuhakikisha wanapitisha wagombea wenye sifa na uwezo wa kunadi sera pamoja na kujenga hoja ndani ya bunge wakati huu ambapo mchakato wa kupata wagombea wa nafasi mbalimbali za ubunge ukiendelea ndani ya chama hicho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Esther Matiko amewataka wagombea kutokuwa na hofu  ya kuwa iwapo watashinda watashindwa  kutanagazwa na kusema wao jukumu lao ni kunadi sera kwa wananchi huku akisisitiza mshikamano miongoni mwao hali itakayosaidia ushindi kupatikana ndani ya chama hicho.

Matiko amewataka watia nia wote wakiwemo wale amabo hawatapitishwa kwenye kura za maoni na kubaki waunge mkono wale watakaochaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho wawe kitu kimoja badala ya kugawanyika.

Naye aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa kambi ya Upinzani Bungeni na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, Esther Bulaya amewataka watia nia wote  wa ubunge Kanda ya Serengeti kusimama imara kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kutoogopa kwani changamoto walizozipitia baadhi ya wabunge wa chama hicho zimewafanya kuimarika zaidi  katika medani ya kisiasa.

Wakati huo huo Chadema Kanda ya Serengeti imetoa vyeti vya pongezi kwa wanachama wake waliokuwa viongozi katika nafasi mbalimbali wakiwemo wabunge, madiwani na wenyeviti wa halmashauri za wilaya ambapo wabunge  hao wameongozwa na Mwenyekiti wao wa kanda aliyekuwa Mbunge waJimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko.

 Naibu Katibu mkuu Chadema Tanzania Bara Bw Benson Kigaila akizungumza na wanachama na watia wa chama hicho kanda ya Serengeti makao makuu yake Mkoani Shinyanga. 
 Mwenyekiti wa Chadema kanda ya  Serengeti Bi Esther Matiko akiwataka wanachama na watia nia kuwa kitu kimoja kabla na baada ya kupatikana kwa wagombea.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara, Esther Bulaya akizungumza na watia nia mbalimbali waliojitokeza katika kikao hicho. 
 Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko  akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Benson Kigaila  kwa ushiriki wake  wa miaka mitano ya ubunge. 
 Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, Benson Kigaila  kwa ushiriki wake wa miaka mitano bungeni.
 Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya    akipokea cheti cha pongezi
Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, Benson Kigaila akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya  Serengeti, Esther Matiko.
Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Zanzibar Salumu Mwalimu (Kushoto) na Naibu katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila (Kulia).
 Wajumbe wa mkutano wa Kanda ya Serengeti wa Kuzungumza na watia nia kanda hiyo wakiendelea kufuatilia mkutano.
 Wanachama na watia nia wakiendelea kufuatilia hotuba ya Naibu katibu mkuu Tanzania Bara.
 Watia Nia ya Ubunge kupitia Chadema Kanda ya Serengeti wakifuatilia kwa ukaribu ujumbe wa  Naibu katibu Mkuu. 

 Waliokuwa wabunge wa Chadema kanda ya Serengeti na Wenyeviti wa halmashauri zilizokuwa chini ya chama hicho wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea vyeti  vya kutambua mchango wao.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464