CHUO KIKUU USHIRIKA MOSHI TAWI LA KIZUMBI CHAWAPIGA MSASA MAOFISA USHIRIKA SIMIYU


 Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi mkoani Shinyanga, Angelina Lucas (kulia) akitoa maelekezo kwa maofisa ushirika.

Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog

Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tawi la kufundishia la Kizumbi mkoani Shinyanga, kimeendesha mafunzo ya namna ya kuandika kisasa vitabu vya mahesabu na kuzifahamu sheria na kanuni za vyama vya ushirika kwa maofisa ushirika ili kuwaongezea uelewa waweze kuvisiadia vyama na wanachama kuelekea msimu huu wa manunuzi wa zao la Pamba.

Mafunzo hayo ya siku tatu yalianza kutolewa Juni 17, 2020 na yamehitimishwa leo Juni 19, mwaka huu kwa maofisa ushirika 13 kutoka wilaya za mkoa wa Simiyu ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa Empire Multipurpose Hotel mjini Shinyanga yakisimamiwa na Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Angelina Lucas akiwaelekeza washiriki

Akitoa mafunzo hayo, Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi, Angelina Lucas, amesema kuwa vyama vya ushirika vilikuwa vinakabiliwa na dhana ya zamani ya usimamizi dhaifu wa rasilimali na kutokuwepo kwa uwajibikaji kutoka kwa viongozi, huku pia kukiwa hakuna watu na wataalam sahihi kwenye vyama hivyo hali iliyopelekea kuwepo kwa vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za wanachama.

"Watumie mafunzo haya kwenda kutatua changamoto kwa wana ushirika kwa sababu iko wazi kwamba ushirika unaiabiliwa na changamoto kubwa ya uandikaji wa vitabu na uandaaji wa taarifa za fedha kwa hiyo maofisa waendelee kujengewa uwezo na wakitumie chuo cha Ushirika Moshi kuimarisha utendaji kazi wao na kuongezewa uelewa," amesema.


Pia Angelina ametoa wito kwa maofisa ushirika kuifahamu sheria ya ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015 ili kuwasaidia kuelewa nini kinatakiwa kufanyika na kuisaidia sekta ya ushirika kupiga hatua.

Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu

Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu ameeleza kuwa wanakabiliwa na uelewa hafifu wa uandaaji wa taarifa za ushirika, usimamizi hafifu wa kumbukumbu za hesabu na uelewa hafifu wa sheria za vyama vya ushirika, hivyo wameamua kutoa mafunzo hayo kwa maofisa ushirika ili kuongeza dhana ya usimamizi na uandaaji wa taarifa, kuondoa dhana ya kufanya kazi kwa mazoea na kupata uelewa wa sheria na kanuni za vyama vya ushirika.
"Uelewa huu utatujengea nguvu ya kwenda kusimamia vyama, kujua na kuyabaini mapema matatizo yanayoweza kujitokeza na kuyachukulia hatua, tunaingia kwenye msimu wa ununuzi wa Pamba kwahiyo tunataka kwenda hatua kwa hatua.

"Sasa kuelekea kwenye huu msimu inapaswa tubadilike kwenye usimamizi na kujiepusha na ubadhilifu, tuache kufanya kazi kwa mazoea tujikite kuwasaidia wananchi wanyonge na tujenge misingi imara ya hivi vyama kumnufaisha mwana ushirika," amesema Kadudu.

Mkoa wa Simiyu unavyo vyama vya ushirika vipatavyo 396, vikiwemo 383 vya Pamba, 12 vya fedha na kimoja cha ufugaji.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Ackiley Athanas ambaye ni Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Maswa, amesema kwamba wanakabiliwa na changamoto ya uandaaji wa kisasa na bora wa taarifa za kifedha (vitabu), hivyo kupitia wao watawafundisha wana ushirika namna ya kuandika na kuifahamu sheria ili kurahisisha kubaini mapungufu na kuyasahihisha.

Washiriki wafuatilia mafunzo kwa umakini mkubwa

Baadhi ya maofisa ushirika kutoka mkoani Simiyu wakielekezana namna ya uandaaji wa vitabu vya mahesabu kisasa wakati wa mafunzo hayo yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Ushirika tawi la Kizumbi Shinyanga.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Abeid Ramadhan akifuatilia mafunzo.

Mafunzo yakiendelea

Mratibu wa mafunzo hayo, Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu.

 Washiriki wakipata ufafanuzi kutoka kwa mkufunzi wao, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Shinyanga, Angelina Lucas (kulia).
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464