HEKARI 100 ZA MASHAMBA YA BANGI ZA BAINIKA MOROGORO





KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, atoa siku mbili kwa viongozi wa vijiji vitano mkoani humo kujisalimisha polisi baada ya operesheni iliyofanywa na jeshi hilo, kubaini hekari 100 za mashamba ya bangi. 
Vijiji hivyo amevitaja kuwa ni Bunduki, Misengere, Kododo, Vinile, na Yowe, kata ya Doma, wilayani Mvomero, vinavyozunguka bonde la Mto Mgeta. 

Kamanda Mtafungwa alitoa agizo hilo jana wakati wa operesheni maalum ya kusaka watu wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu vya kuzalisha na kuuza bangi kinyume na sheria.

Alisema mashamba hayo zaidi ya hekari 100 yamebainika umbali wa kilomita 30 kutoka eneo la makazi ya watu katika kijiji cha Misengele, Tarafa ya Doma.

“Natoa siku mbili kwa viongozi hawa wa jijiji kujisalimisha kituo cha polisi wenyewe ili watuambie walikuwa wapi miaka yote mambo haya yanafanyika katika maeneo yao pasipo kutoa taarifa yoyote,” alihoji Mutafungwa.

Alisema eneo hilo lililopo karibu na mto Mgeta, lipo ndani ya hifadhi ya msitu asilia wa Misengele na kuzitaka mamlaka zinazohusika na uhifadhi wa maeneo hayo kuweka uangalizi wa karibu kujua shughuli zinazoendelea.

“Eneo hili ni hifadhi hairuhusiwi mtu yeyote kufika ama kuendesha shughuli za kibinadamu, lakini katika operesheni kufuatilia taarifa za uchunguzi inabainika uwapo wa mashamba haya makubwa ilhali viongozi wa vijiji wapo na wamenyamaza,” alisema SACP Mtafungwa.

Kamanda Mtafungwa alisema katika operesheni hiyo inayoendelea watu 12 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Doma, Mapambano Mkopi, aliyeshiriki katika operesheni hiyo, alisema walishindwa kutambua uwapo wa shughuli hizo kutokana na umbali toka yalipo makazi ya watu.
CHANZO - NIPASHE
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464