Jengo la kisasa la kukaa wananchi wanaofika kusubiri kuona wagonjwa ndugu na jamaa wanaolazwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama ambalo limejengwa kwa msaada wa makampuni ya muwekezaji mzawa ya Kahama Oil Mill kwa gharama ya Sh milioni 11.8 pamoja na kuweka mabechi ya kukaa watu.
Na Patrick Mabula - Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Anamringi Macha ameipongeza Kampuni ya Kahama Oil Mill (KOM) inayomilikiwa na mwekezaji mzawa kwa hatua ya kujenga jengo la kisasa la kupumzikia wananchi wanaofika katika hospitali ya wilaya hiyo kuwajulia hali wagonjwa.
DC Macha ametoa pongezi hizo jana Jumatatu mjini Kahama wakati akifungua jengo hilo na kueleza kuwa uwepo wa jengo hilo ni msaada kwani utawaondolea adha wananachi kukaa juani na wakati wa masika kunyeshewa na mvua wanapofika kuona wagonjwa ndugu na jamaa zao waliolazwa hospitalini hapo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Lucas David alisema hospitali hiyo ilikuwa inakabiriwa na changamoto ya sehemu ya kukaa wananchi wanaofika hapo kusubiri kuona na kusalimia wagonjwa wao, ambapo walikuwa wanakaa barabarani juani na wakati wa masika kunyeshewa na mvua kwa msaada huo kero hiyo itakwisha.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Clemenc Mkusa alishukuru kampuni ya KOM kwa kuona kero hiyo iliyokuwa inawapata wananchi, huku akieleza kuwa hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto nyingi za kuboresha huduma ya afya na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia sekta hiyo.
Meneja Mahusiano wa makampuni ya KOM, Brayson Edward alisema walibaini kero hiyo na kuiomba halmshauri kibali cha kusaidia msaada huo ambao ulikubalika haraka na walianza ujenzi mara moja na hadi kukamilika wametumia Sh Milioni 11.8 pamoja na kuweka mabechi ya kukaa wananchi wanaofika hapo kusubiri saa ya kuona wagonjwa wao.
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (katikati) akizungumza na wananchi baada ya kufungua jengo la kisasa la kukaa wananchi kusubiri kuona na kusalimia ndugu na jamaa wagonjwa wao waliolazwa katika hosptali ya wilaya hiyo lililojengwa kwa msaada wa makampuni ya Kahama Oil Mill (KOM ), kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Clemenci Mkusa na kulia ni Meneja wa KOM, Brayson Edward.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Clemenci Mkusa (aliyesimama) akishukuru kwa msaada wa kujengewa jengo la kukaa wananchi wanaofika katika hospitari ya wilaya hiyo kuona wagonjwa.
Meneja Mahusiano wa makampuni ya Kahama Oil Mill (KOM ), Brayson Edward (kulia) akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo la kukaa wananchi wanaofika hospitali ya wilaya ya Kahama kuona wagonjwa lililojengwa na kampuni hiyo kwa Sh Milioni 11.8.
Picha Zote na Patrick Mabula