Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amethibitisha kukamatwa kwa kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe, mkoani Lindi Kusini mwa Tanzania.
Zitto ana ziara ya siku tatu kusini mwa Tanzania, kutembelea majimbo mbalimbali anapokea madiwani wanaotaka kujiunga na chama chake ambao wamemaliza muda wao.
''Jana alikuwa katika jimbo la Rufiji na alipokea madiwani wanne kwa kikao cha ndani, leo alikuwa katika jimbo la Kilwa Kusini ambako alienda kumpeleka mbunge Suleiman Bundala maarufu Bwege ambaye hivi karibuni alijiunga na chama chetu na madiwani wanane wa chama cha wananchi CUF ambao nao wamejiunga walikuwa wanatarajiwa kupokelewa leo kwa kutumia kikao cha ndani ambao ni taratibu za kawaida za chama''.
Akizungumza na BBC, Bwana Shaibu amesema majira ya saa sita mchana polisi walivamia kikao hicho na kumkamata zitto Kabwe na viongozi mbalimbali wa mkoa na wa jimbo la Kilwa Kusini pamoja na mbunge Suleiman Bundala ambao bado wanashikiliwa na polisi katika kituo cha polisi wilayani Kilwa.
Bwana Shaibu amesema kuwa hili si tukio la kwanza kwa polisi kuingilia mikutano ya ndani ya chama , na shughuli za kisiasa ambazo ni halali kabisa kisheria.
Kiongozi huyo amelaumu kuwa Jeshi hilo linafanya vitendo hivyo kwa manufaa ya serikali iliyo madarakani badala ya kutumika kwa maslahi ya Umma.
Amesema kuwa pamoja na tukio hilo chama cha ACT Wazalendo kitaendelea na ratiba zake kama ilivyo kawaida yake kwa mujibu wa sheria, kwa kuwa chama kina uhuru wa kuendelea na shughuli za kisiasa.
Akizungumzia kuhusu matukio mbalimbali yanayojitokeza nyakati mbalimbali za uchaguzi, ado amesema '' kuna matendo kadha wa kadha ambayo yanaondosha dhana nzima ya demokrasia nchini '' akionya kuwa hawatakubali iwapo mamlaka hazitazingatia misingi ya haki na Demokrasia. ''Tutarudi kwa Umma na kuhakikisha tunasimama nao ili haki yetu ipatikane''.
''Katiba yetu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria mbalimbali za nchi zimetoa haki kadha wa kadha ambazo mtu anaweza kuzitumia kuhakikisha kuwa haki yake inalindwa, kutetewa na kupatikana, ninavyosema kuwa tutarudi kwa Umma maana yake ni kuwa tutafanya hivyo kwa misingi ya kisheria na si kinyume cha sheria.'' Alisema bwana Shaibu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464