Maalim Seif Sharif Hamad
KWA mara nyingine Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza nia ya kugombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Act-Wazalendo ikiwa ni mara ya sita kugombea nafasi hiyo toka mwaka 1995.
Akizunguma na waandishi wa habari jana Mjini Zanzibar, alisema amefikia uamuzi huo kutokana na sababu tano zilizomsukuma ikiwamo kutoridhishwa na jinsi nchi inavyoendeshwa.
“Kwa kuzingatia hatari hii nimeona ni hekima kukubali ushauri wa watu wengi kwamba huu si wakati wa kuacha mapambano bali ninawajibu kushirikiana na viongozi na vijana kuwavusha katika wakati huu mgumu katika historia ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla," alisema.
Alitaja sababu nyingine kuwa mwaka 1992 yeye na wenzake waliamua kuanzisha Chama cha CUF na kuwashawishi wananchi kukiunga mkono ambacho kilikuwa na malengo ya wazi ya kurejesha haki bila ya ubaguzi, kupinga ukandamizaji na nchi kukwama.
Alisema hali hiyo ilikuwa ni mwiba kwa watawala wasiopenda kuiona Zanzibar ikikwamuka kimaendeleo na ndipo wakaamua kutumia dola kukidhoofisha chama hicho na hatimaye kufukuzwa kwenye chama kinyume cha matakwa ya wanachama.
Alieleza kuwa yeye ni nahodha mzoefu kwa kuliongoza jahazi, hivyo amekubali kuliongoza jahazi la kuleta mabadiliko kupitia ACT-Wazalendo.
“Katika hali hii nimeona haitokuwa busara ikiwa nahodha mzoefu wa kuongoza watu kuingia katika jahazi jipya halafu kuwaacha mkondoni…nimekubali ushauri kuwa niongoze juhudi za kuleta mabadiliko kupitia ACT -Wazalendo hasa wakati huu nchi yetu inapoelekea kuandika historia mpya,” alisema.
Maalim Seif alisema jahazi jipya linahitaji nahodha mwenye uzoefu mkubwa aweze kuivusha Zanzibar kupisha dhoruba kali na yenye mawimbi mazito yanayoikabili.
Alieleza kuwa viongozi na wanachama wa chama hicho wamemwamini kupeperusha bendera ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar.
Alisema ameona si uungwana hata kidogo kudharau imani hiyo na badala yake anapaswa kuheshimu kwa kuwaongoza Wazanzibari kufikia ndoto ya Zanzibar wanayoitaka.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464