MASHABIKI WARUHUSIWA KESHO SOKOINE MBEYA, SIMBA IKITARAJIWA KUBEBA UBINGWA VPL



Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog

SIKU tatu baada ya Serikali kupiga marufuku mashabiki kuingia uwanjani katika michezo yote ambayo itazihusisha Klabu za Simba na Yanga katika viwanja vya nje ya Dar es Salaam ukiwemo uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, hatimaye zuio hilo limeondolewa na sasa mashabiki wataruhusiwa kuhushuhudia mchezo wa kesho Juni 28, 2020 utakaozikutanisha Prisons na Simba, mkoani Mbeya.

Alhamisi Juni 25, 2020 Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliizuia Klabu ya Mbeya City kuruhusu mashabiki kuhudhuria katika michezo yake ya nyumbani kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya kufuatia kukiuka masharti na kanuni za afya juu ya kujikinga na Virusi vya Corona kwenye mchezo wao dhidi ya Simba SC uliopigwa uwanjani hapo Juni 24, 2020 (Jumatano) ukimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Ambapo kesho katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, wenyeji Prisons watawakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Simba SC, huku mchezo huo ukitazamiwa kuhudhuriwa na mashabiki kibao pia ukitolewa macho na wadau mbalimbali wa soka nchini kwani Simba wanatarajia kutangaza ubingwa wao wa tatu mfululizo wa VPL.
Mpaka sasa Simba wanaongoza ligi hiyo wakiwa na alama 78 baada ya kushuka dimbani mara 31 wakibakiza michezo saba pekee, huku mpinzani wake Azam FC akifuatia kwa mbali na pointi zake 58 na Yanga akiwa kwenye nafasi ya tatu na alama 57.

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Juni 27, 2020 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shamimu Nyaki alisema japokuwa mashabiki wameruhusiwa lakini endapo kutakuwa na uvunjifu wa masharti basi uwanja huo utachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufungiwa kabisa kutumika kwa michezo ya ligi kuu.

SOMA ZAIDI TAARIFA HIYO HAPA CHINI









Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464