Header Ads Widget

AKAMATWA NA POLISI AKITOROKA KWENDA NCHINI KENYA BAADA YA KUKEKETA WATOTO 10





        Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah

JESHI la Polisi Mkoani Mara limemkamata mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mary Onyango (50) maarufu Kwa jina la Mgesi Mwita Mkazi wa Kitongoji Cha Nyahende Wilayani Serengeti Mkoani Mara anayedaiwa kuwakeketa watoto wa kike 10 akishirikiana na wazazi wao na kisha kukimbia kujificha nchini Kenya.

Akizungumzia kukamatwa kwa mwanamke huyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah, amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa na maofisa wa Polisi Kitengo cha Upelelezi kutoka Serengeti Juni 12, mwaka huu saa mbili za asubuhi eneo la Sirari Wilayani Tarime.


Amesema baada ya kukamatwa amesafirishwa mpaka Kituo cha Polisi cha Serengeti ambapo anaendelea kuhojiwa na baadaye atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Baada ya kufanya matukio ya kukeketwa wasichana hao, alijua Polisi wanamtafuta na ndipo alipokimbilia nchini Kenya kujificha, lakini ameendelea kutafutwa na Polisi na kufanikiwa kukamatwa.

Baada ya kuhojiwa atafikishwa mahakamani, ingawa kwa sasa kesi tatu zipo mahakamani ambazo zinamhusu yeye na baadhi ya wazazi ambao tayari walikamatwa kuhusiana na kitendo hicho kisichofaa kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema.