MHANDISI MASAUNI AREJESHA FOMU, WAGOMBEA URAIS ZANZIBAR WAFIKA 30

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni akikabidhi leo fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni leo amerudisha fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar

Mhandisi Masauni anafanya idadi ya wagombea waliorejesha fomu hizo kufikia 14 hadi leo Juni 27, 2020

Wengine ambao tayari wamekwisharejesha fomu ni Profesa Makame Mbarawa, Shamsi Vuai Nahodha na Ayoub Mohammed Mahmoud, Mohammed Hija Mohammed, Mbwana Bakari Juma na Abdulhalim Mohammed Ali.

Makada wengine waliorejesha fomu kabla ya jana ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Balozi Ali Karume na Hamis Mussa Omari. 

Jumla ya wagombea ya waliochukua fomu ya kuomba kuwania urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefikia 30, ambapo kati ya hao wanawake ni watatu, wanaume 27 wakiwemo watoto watatu wa marais wastaafu. 

Hatua ambayo imezidi kuufanya mchakato huo kuwa mgumu hasa kwa upande wa waliojitokeza ambao wana sifa zinazojieleza. 

Watoto watatu wa marais wastaafu waliojitokeza kuchukua fomu kwenye mchakato huo ni Mussa Aboud Jumbe mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe, pia wamo Dk. Hussein Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Dk. Ali Hassan Mwinyi na Balozi Ali Abeid Karume ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume. 

Wanawake waliojitokeza ni Mwatum Mussa Sultan, Hasna Atai Masoud na Fatma Kombo Masoud. 

Zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu, sambamba na utafutaji wadhamini lilifunguliwa Juni 15 mwaka huu, ambapo linatarajiwa kufika tamati Juni 30, mwaka huu saa 10:00 jioni, ambapo baada ya hapo wanachama waliotia nia watasubiri hatua inayofuata ya uchujaji ili kupata idhini ya kuingia katika mchakato wa kumrithi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, anayemaliza kipindi cha uongozi wake wa miaka 10 tangu achaguliwe mwaka 2010. 

Orodha ya Wagombea waliochukua fomu 

Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohammed Jaffar Jumanne, Mohammed Hijja Mohammed, Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa. 

Wengine ni Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohammed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk. Khalid Salum Mohammed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni, Mohammed Aboud, Bakar Rashid Bakari, Hussein Ibrahim Makungu, Ayoub Mohammed Mahmoud, Hashim Salum Hashim pamoja na Hasna Attai Masoud. 

Picha Mbalimbali zikimwonyesha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhandisi Hamad Masauni akirejesha fomu leo Juni 27, 2020




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464