MWANAMKE AUAWA KWA KUPIGWA MAWE KISA TUHUMA ZA USHIRIKINA



JESHI la Polisi mkoani Rukwa linawasaka watu wasiojulikana kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga mawe, mwanamke aliyefahamika kwa jina la Maria Birika (40), mkazi wa Kijiji cha Myunga, Kata ya Mkali, wilayani Kalambo.
Imeelezwa kuwa watu hao wamemfanyia kitendo hicho kwa kumtuhumu kujihusisha na vitendo vya kishirikina.

Tukio la mauaji ya mwanamke huyo lilitokea Juni 26, saa 12:00 jioni baada ya watu hao kufika nyumbani kwake na kumkuta mtoto aliyefahamika kwa jina Given Lameck (15), akiwa amefungiwa nyumbani kwa mwanamke huyo, huku akiwa amefungwa kitambaa chekundu usoni.

Kabla ya mauaji hayo, mtoto Given alipotea nyumbani kwao katika mazingira ya kutatanisha, ndipo harakati za kumtafuta zilianza, na kwamba ndugu zake walimtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo, alisema baada ya jitihada za kumpata mtoto huyo kushindikana, waliamua kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji kisha kuendelea kumtafuta.

Alisema baada ya kumtafuta kwa muda mrefu walifanikiwa kumkuta nyumbani kwa mwanamke huyo akiwa amefungiwa ndani na amefungwa kitambaa chekundu usoni, huku akionekana kana kwamba amechanganyikiwa kutokana na kuongea vitu visivyoeleweka.

Baada ya kupatikana kwa mtoto huyo, ndipo watu waliokuwa wakimtafuta walipo hamaki na kushikwa na hasira na kuanza kumpiga mwanamke huyo kwa mawe na vipande vya matofali vilivyokuwa karibu na nyumba yake na kumsababishia majeraha makubwa, kuvuja damu nyingi na kufariki dunia kutokana na kukosa matibabu ya haraka.

Kamanda Masejo alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Rukwa kuachana na imani za kishirikina katika matukio yanayotokea mkoani humo, kwa kuwa imani hizo zimekuwa chanzo cha vifo vingi vinavyotokana na kujichukulia sheria mikononi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464