MZABUNI ADAKWA NA TAKUKURU KWA KUWEKA MADIRISHA YALIYO CHINI YA KIWANGO IKULU NDOGO



Nembo ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru)

Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog

OFISI ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara inamshikilia Patrick Joakimu Kauky (Gaudensi Joakimu Kauki) baada ya kubainika kuweka madirisha yaliyo chini ya kiwango katika ujenzi wa Ikulu ndogo unaoendelea wilayani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 22, 2020 kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Holle Makungu imesema kuwa uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo ulibaini kuwa mzabuni huyo alipewa zabuni ya kutengeneza madirisha ya Alminium na ofisi ya manunuzi mkoa wa Manyara kwa jengo la Ikulu ndogo inayojengwa wilayani Hanang'.

Hata hivyo uchunguzi unaonyesha pia mzabuni huyo alipewa kandarasi hiyo na idara ya manunuzi mkoani humo kinyume na sheria ya manunuzi ya umma.

Ambapo kwa mujibu wa BOQ, mzabuni alitakiwa kutengeneza na kuweka kwenye jengo hilo madirisha ya Alminium yenye kioo cha unene (thickness) ya 6mm lakini badala yake akatengeneza na akapeleka eneo la ujenzi madirisha yenye kioo cha unene wa 5mm.

"Katika ufuatiliaji wa mradi huo ikiwa ni moja ya majukumu yetu kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2017, Takukuru wilaya ya Hanang' walibaini dirisha hizo ziko chini ya kiwango kilichoainishwa na BOQ.

"Baada ya kubaini hilo, Takukuru Hanang' walichukua hatua za kumuagiza mzabuni asiyatumie madirisha hayo kwenye jengo hilo hadi atakapoleta madirisha ya kiwango kilichobainishwa katika BOQ na kufanyiwa ukaguzi ili kujiridhisha na ubora kama ambavyo tunafanya kwenye miradi mingine," amesema.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Holle Makungu

Makungu ameeleza kuwa Mzabuni huyo alimweleza zuio hilo Mhandisi wa mkoa, Eng. Dominicianus Kilina kwa njia ya simu ambaye bila hata ya kuwasiliana na Takukuru alielekeza madirisha hayo yafitishwe yakiwa hivyo hivyo haraka haraka na mzabuni huyo.

"Takukuru mkoa wa Manyara tulipata taarifa hiyo ya kudharau maelekezo yetu na nikaelekeza mzabuni na mafundi wake wote waliokutwa wanatekeleza agizo la mhandisi huyo wakamatwe kwa uchunguzi wakati mhandisi Kilina akitafutwa kusaidia uchunguzi huo, Kilina bado hajapatikana kwa kuwa tulielezwa kuwa yuko nje ya Babati kikazi," amesema.

Makungu ametoa rai kwa watendaji walio chini ya ofisi ya katibu tawala mkoa wa Manyara kukubali kuwa sehemu ya vita dhidi ya Rushwa na kila mmoja kutekeleza wajibu wake ili kufanikisha vita hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464