Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amepiga marufuku watu wanaofanya biashara nje ya mfumo wa masoko yaliyoanzishwa maarufu kama vishoka na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Naibu Waziri Nyongo ameyasema hayo mapema leo Juni 29, 2020 kwenye mkutano wake na wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Tunduru ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye soko hilo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye uendeshaji wa soko hilo.
Katika kikao hicho Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Ruvuma, Isaack Ngerangera, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Getty Massawe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephraim Mushi na Afisa Utawala wa Tume ya Madini, Saashisha Mafuwe.
Amesema kuwa, katika Soko la Madini la Tunduru wapo watu wasio waaminifu wamekuwa wakifanya biashara ya madini nje ya soko la madini lililoanzishwa na kuongeza kuwa Serikali haitawafumbia macho kwa kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi kutokana na kukwepa kodi mbalimbali zinazotakiwa kulipwa Serikalini.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inakuja na mkakati mpya wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa madini wanatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa.
Wakati huohuo, Naibu Waziri Nyongo amemsimamisha kazi aliyekuwa Mkaguzi Msaidizi wa Madini, Athumani Masawe ambaye alituhumiwa na wanunuzi wa madini kuhusika na kufanya biashara nje ya soko kinyume na sheria ya madini.
Katika hatua nyingine Nyongo amesema kuwa ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wananufaika na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliamua kufuta kodi nyingi zilizokuwa kero kwa wachimbaji wa madini pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini.
Katika hatua nyingine, Nyongo amewataka maafisa madini wakazi nchini kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama na Taasisi nyingine za Serikali.
Aidha amekemea vikali tabia ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wilaya ya Tunduru kuingilia shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini ndani ya Soko la Madini la Tunduru.
Katika hatua nyingine alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwenye sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wilaya ya Tunduru kwa kuingilia shughuli za uendeshaji wa Soko la Madini la Tunduru.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amempongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kufanya ziara kwenye soko hilo na kutatua changamoto zilizojitokeza na kuongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma kwenye usimamizi wa Soko la Madini Tunduru ili liwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.
Tazama picha mbalimbali hapa chini za mkutano wa Naibu Waziri Nyongo na wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Tunduru
Picha zote na Grayson Mwase - Afisa Habari Tume ya Madini
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464