JPM: TUSIDHARAU DAWA ZA KIENYEJI, KUJIFUKIZA KUMETUSAIDIA SANA







Rais John Magufuli akizungumza leo jijini Dodoma.


Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ametoa wito kwa watanzania kutodharau dawa za kienyeji zinazopatikana nchini, huku akitoa maagizo kwa wizara husika kuziendeleza ziweze kuwasaidia wananchi.

Rais Magufuli pia amewapongeza viongozi wa dini zote nchini kwa kuungana na serikali katika kufanya maombi mbalimbali ya kudhibiti Corona, huku akieleza kuwa hatua zilizochukuliwa na watanzania za kujifukiza zimesaidia sana kupunguza maambukizi ya virusi hivyo nchini.

Ameyasema hayo leo Juni 11, 2020 jijini Dodoma katika hafla ya kuzindua jengo la ofisi za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), kukabidhi pikipiki kwa maofisa tarafa na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 51.2 ya kiwango cha lami katika mji wa kiserikali Mtumba, Dodoma.

"Dawa za asili hazijapitwa na wakati bali anayesema hivyo ndiye amepitwa na wakati, wale wote wanaotengeneza dawa za asili tuwasapoti, kila nchi hata Ulaya wana dawa zao za asili, niwaombe Watanzania na Wizara zinazohusika tusidharau vyetu bali tuviendeleze. Huku kujifukiza kumetusaidia sana, Corona haijaisha sana Tanzania lakini imepungua sana," amesema.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini kwa kuungana na Serikali na kuliombea taifa katika kipindi kigumu cha maambukizi ya Virusi vya Corona, ambapo amewaomba Watanzania kupuuza propaganda zinazoenezwa na maadui wasiolitakia mema taifa bali waendelee kuchapa kazi.
"Waliotegemea tutakufa na kuzagaa mitaani wameshindwa na wamelegea, Mungu wetu anatupenda sana.Watazungumza mengi na watu wao wanaowatumia watazungumza mengi, nyie endeleeni kuchapa kazi, tulimuomba Mungu na ametusaidia, Mungu hamtupi mtu anaemuomba ndiye mwenye huruma ya kweli," amesema Rais Magufuli.





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464