Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akizungumza na madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakati wa kikao cha baraza la madiwani kujadli hoja mbalimbali za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) leo Alhamisi Juni 4, 2020.
Na Damian Masyenene – Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameonyesha
kukasirishwa na kitendo cha baadhi ya watumishi wa serikali Halmashauri ya
Wilaya ya Shinyanga kukaidi maelekezo ya kuondoka mjini (Manispaa) na kuhamia
eneo la kazi ilipo halmashauri yao (Iselamagazi).
Ambapo kufuatia kitendo hicho, Mkuu huyo wa mkoa amewapa saa
tano kuanzia saa 7:00 mchana hadi 12:00 jioni siku ya Alhamisi Juni 4, 2020
wawe wameondoka na kuhamia kwenye vituo vyao vya kazi vinginevyo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
RC Telack ametoa maagizo hayo leo Juni 4, 2020 wakati wa
kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichoketi kupitia hoja
mbalimbali za Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), ambapo kupita kikao
hicho aligundua kuwa baadhi ya wakuu wa idara na vitengo hawakuwepo kutokana na
kukaa mbali na eneo la kazi.
Hivyo, RC Telack alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,
Hoja Mahiba kumletea orodha ya majina ya watumishi hao na idara za kazi
wanazotoka kama hawataripoti/kuhamia Iselamagazi itakapofika kesho (Ijumaa) asubuhi,
huku pia akimtaka awasilishe orodha ya majina ya watumishi wote ambao
hawakuhudhuria kikao hicho wala kujiandikisha kwenye daftari la mahudhurio.
“Wamekaidi maelekezo ya Rais na wanataka kunijaribu, kwahiyo Mkurugenzi
naagiza watumishi wote wanaokaa mjini kufika leo jioni wawe wamehamia hapa
(Iselamagazi), ambao hawatahamia nataka kesho asubuhi uniletee majina na idara
walizopo.
“Pia watumishi wote ambao hawapo na hawajajisajili kwenye Kitabu
cha mahudhurio na wako mjini nataka majina yao, namba za simu na idara
wanazotoka,” amesema Mkuu wa Mkoa.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakifuatilia kwa umakini hoja mbalimbali wakati wa kikao cha kujadili ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) leo Alhamisi Juni 4, 2020.
Katika upande mwingine RC Telack aliwataka watumishi wote
katika halmashauri hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano, kuvunja makundi na kumpa
ushirikiano Mkurugenzi, Hoja Mahiba na waachane na propaganda za kutaka
aondolewe.
Akizungumzia maagizo ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Shinyanga, Hoja Mahiba, ameyapokea maelekezo hayo na yatafanyiwa
kazi mara moja, huku akiwataka watumishi wake kurudi kwenye msitari na
kuyatilia maanani yale yote yaliyoelekezwa kwenye kikao hicho.
“Nimepokea maelekezo nitayasimamia ili halmashauri yetu iweze
kwenda kwenye msitari unaotakiwa, kwa watendaji wangu nawaambia mwenye masikio
na asikie na wajipange kurudi kwenye msitari kama walikuwa wamekengeuka,”
amesema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga (RAS),
Albert Msovela alisema tatizo la watumishi kukatalia mjini limekuwa sugu kwa
halmashauri hiyo, ambapo baadhi ya watumishi wamekuwa wakidanganya kuwa
wameenda likizo lakini wanapita kwenye vyanzo vya mapato wanakusanya fedha na
hawazifikishi kwenye halmashauri hiyo.
“Baadhi ya watumishi bado wanakatalia mjini hawataki kuhamia
huku, naagiza Mkurugenzi wakuu wa idara wawe na madaftari ya mahudhurio kuwaona
wasaidizi wao, wengine wanasema wameenda likizo kumbe wanazurura kukusanya
fedha na hazifiki kwenye halmashauri,” amesema.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
hiyo, Ngassa Mboje alimuomba Katbu Tawala wa Mkoa kuwasaidia kutatua tatizo la
upungufu wa madereva wa halmashauri, ambapo kwa sasa wapo 10 peke yake wakati mahitaji
ni 21.
“Naomba watumishi turudi kwenye utaratibu siyo vyema tukiwa tunasemana kila siku, tumuombe RAS aendelee kufanya vikao vya kila mara na watumishi kukumbushana wajibu na maeneo ambayo hatujafanya vizuri tuyachukue kama changamoto,” amesema.