Picha kwa hisani ya UNICEF Tanzania
Kutokana na uwepo wa uvumi na taarifa za baadhi ya shule kuwataka wanafunzi kwenda na Barakoa shuleni, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa taarifa ya ufafanuzi kwa Umma jana Juni 28, 2020 kuhusu matumizi ya Barakoa kwa wanafunzi.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (Afya), Gerald Chami ilisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushauriana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, ilitoa Mwongozo wa Pili (25 Juni 2020) wa udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa CORONA (COVID-19) kwa wanafunzi.
Ambapo pamoja na kutolewa elimu kuhusiana na mwongozo huo, Wizara imetoa ufafanuzi zaidi juu ya matumizi ya Barakoa kwa wanafunzi ili kueleweka vizuri kwa wanafunzi, walimu na wananchi. sehemu ya maelekezo hayo ni haya yafuatayo;
1. Mwongozo unaelekeza wanafunzi watumie Barakoa katika mazingira ya Msongamano
2. Wanafunzi katika makundi yafuatayo wanaelekezwa wasitumie Barakoa kabisa; a) Watoto wote waliochini ya umri wa miaka minane (8) b) Wanafunzi wote (hata kama ana zaidi ya miaka 8) wenye matatizo ya kiafya kama vile magonjwa ya Mfumo wa Upumuaji mfano Pumu (Asthma), matatizo ya Moyo, Selimundu (Sickle Cell Disease) na wale ambao historia yao katika uongozi wa shule inaonyesha wana matatizo ya kiafya yanayoweza kuathiri upumuaji.
Aidha, wanafunzi hawapaswi kuvaa barakoa wakati wa michezo au wakiwa wanafanya mazoezi mengine ikiwemo kukimbia mchakamchaka Wanafunzi wenye kisukari, shinikizo la damu, unene mkubwa na wenye matatizo ya figo, wavae lakini wafatiliwe kwa uangalizi wa karibu. Walimu wa Madarasa na Walimu wakuu wanaelekezwa kuwa karibu na wanafunzi katika kufuata maelekezo ya mwongozo huu na kutoa taarifa mapema pale ambapo mwanafunzi anapopata shida yoyote kama kupumua, kuishiwa nguvu au kukohoa.
"Pamoja na uzoefu wa kisayansi tunaoupata kuhusiana na ugonjwa huu, na kwa kuzingatia mazingira yetu, Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu sana utekelezaji wa Mwongozo kuhusu matumizi sahihi ya Barakoa kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na changamoto zinazojitokeza.
"Aidha, Wadau wa elimu, wazazi na walezi wanakaribishwa kutoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa mwongozo huo iwapo italazimika kuboreshwa ili kuwalinda wanafunzi," ilisema taarifa hiyo