SERIKALI YAWAKUMBUKA WAJANE, YAELEZA HATUA ZILIZOPIGWA KUWAINUA


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Grace Mwangwa (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ambayo huadhimishwa kila Juni 23. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Mwajuma Magwiza na kulia ni Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA), Rose Sarwatt. 

Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali imesitiza umuhimu wa kuendelea kutatua kero zinazoyakabiri makundi maalum katika jamii wakiwemo Wajane, mama lishe na wauza mboga kwa kuwapatia maeneo rasmi ya kufanyia biashara ili kujikwamua katika hali ya utegemezi na na hivyo kuboresha kipato.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika hotuba yake kuhusu maadhimisho ya siku ya wajane Duniani iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Grace Mwangwa leo Juni 22, 2020 jijini Dodoma.

Amesema kuwa Serikali imetenga maeneo yenye ukubwa wa hekta 15,800 katika Halmashauri 150 nchini ili kukuwawezesha wajane na makundi mengine kufanya shughuli za kujiingizia kipato na mhivyo kuboresha uchumi.

Ameongeza kuwa Serikali imefuta ada na tozo 108 kati ya 139 ikilenga kupunguza kero kwa makundi hayo maalum wakiwemo wajane ambao imesema ni kundi muhimu katika msingi wa maendeleo ya nchi.

Mwangwa amefafanua kuwa Serikali imetoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake wakiwemo Wajane kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 63.49 iliyotolewa kwa wanawake wajasiriamali 938,802 kupitia asilimia 4 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Katika jitihada za kuhakikisha haki za wanawake zinalindwa, Kuwepo kwa mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWA 2017/18 – 2021/2022) mpango unaolenga kutokomeza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Kwa kutambua umuhimu wa Siku ya Wajane Duniani, Serikali imewahamshisha wadau kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili wajane kama zinavyobainishwa katika sera mbalimbali ambazo ni pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), Maazimio ya ulingo wa Beijing, Ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Ajenda ya Maendeleo ya bara la Afrika 2063.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu idadi ya wajane nchini Tanzania ni laki 8.8 sawa na asilimia 3.1 ya wanawake wote Nchini ambao hadi mwaka 2019 walikadiriwa kufikia millioni 28.5.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA), Rose Sarwatt amesema Wajane wasijifiche na kujiona wanyonge bali wajitokeze na kueleza matatizo yao kwa mamlaka mbalimbali wakiwemo Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Kata ili kuweza kupatiwa msaada stahiki.

Mmoja wa wajane walioshiriki katika mkutano huo, Edina Mkhandi ameiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa kesi za wajane zinapopelekwa mahakamani ili kwasaidia wajane hao kupata haki zao kwani wamekuwa wakinyanyasika sana katika kupata haki zao za mirathi na watoto.

Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yanayoadhimishwa kila Juni 23 yanaenda kwa Kauli mbiu “Haki na Ulinzi kwa Wajane: Msingi Imara kwa Maendeleo ya Jamii” ambayo inasisitiza jamii na wadau kuzingatia haki na ulinzi wa wajane katika nyanja mbalimbali.
Mkurugenzi wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA), Rose Sarwatt (kulia) akieleza namna Chama hicho kinavyowasaidia Wajane Tanzania kuondokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za Mirathi wakati wa Tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu liliotolewa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia,Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Grace Mwangwa (kushoto) leo Jijini Dodoma.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464