LICHA ya kutoka suluhu ya bila kufungana na wenyeji wao Tanzania Prisons katika mchezo uliochezwa leo jioni katika Uwanja wa Sokoine, timu ya Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) kwa msimu wa tatu mfululizo.
Suluhu hiyo ambayo ya pili kwa timu hizo msimu huu, imewafanya Simba kufikisha pointi 79 ambazo hatitoweza kufikiwa na timu yoyote katika Ligi huku pia wakiwa wamesalia na mechi sita mkononi.
Baada ya kutwaa ubingwa huo sasa vita kubwa ipo kwenye nafasi ya pili ambayo inawaniwa na Yanga wenye pointi 60 na Azam waliofikisha pointi 59 zote zikiwa zimecheza mechi 32.
Katika mchezo huo uliochezesha na mwamuzi wa kati Abubakar Mturo akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja, Janeth Balama na Paschal Joseph, wenyeji Prisons walionekana kubaini mapema mbinu za wapinzani wao na kuwadhibiti vilivyo.
Prisons walifika mara kadhaa langoni kwa Simba lakini uimara wa kipa Aishi Manula na walinzi wake waliokoa mashambuliai huku pia mara kadhaa washambuliaji wa Simba nao wakimjaribu kipa Jeremiah Kisubi bila mafanikio.
Kwa upande wa Simba unaweza kusema walichokihitaji ni sare katika mchezo huo kutokana na kikosi walichokiingiza kwani hata kabla ya mchezo malengo yao ilikuwa kuchukua alama moja pekee ambayo itawapa ubingwa wa tatu mfululizo.
Kocha mkuu wa timu hiyo Sven Vandenbroeck alionekana kuwapumzisha nyota wake muhimu ambao huenda tukaona wakaanza katika mchezo wao wa Julai Mosi dhidi ya Azam FC katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup).
Katika mashindano hayo ambayo Simba atakutana na Azam katika hatua ya Robo Fainali, atakutana na upinzani mkali kutokana na Azam kutaka kutetea ubingwa wao na kuiwakilisha tena nchi katika mashindano ya kimataifa baada ya msimu huu kutokuwa mzuri kwao baada ya kutolewa kwenye hatua za awali sawa na Simba ambao walikuwa wakiiwakilisha nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa.
Si Simba na Azam pekee wanaolihitaji kombe hilo bali timu zote zilizoingia hatua hiyo ikiwemo Yanga, zimetamba kufanya maajabu na kuhakikisha wanafanya kila liwezekanalo kutwaa taji hilo.
Vandenbroeck ambaye mara kadhaa amekuwa akisema kuwa lengo lake kubwa ni kuhakikisha anatetea taji la Ligi kwa msimu wa tatu mfululizo lakini pia aliwahi kuwahakikisha mashabiki kuwa watafanya vizuri katika hatua ya robo fainali ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele na kutwaa taji hilo.
Kabla hata ya kocha huyo huyo kuweka wazi nia yake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji alikuwa anatamani kukutana na wapinzani wao Yanga katika hatua ya robo Fainali ili kulipa kisasi baada ya kuwafunga goli 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi uliochezwa Machi 8.
Baada ya mchezo huo Dewji pamoja na viongozi wa wapinzani wao Yanga tayari walishaanza kikakati ya kuhakikisha wanatwaa kombe hilo ili kujihakikishia nafasi ya kurudi kwenye mashindano ya kimataifa huku wadhamini wao kampuni ya GSM wakisema wapo radhi kuweka mezani dau nono zaidi hata ya lile milioni 200 walilotoa Machi 8 ili kuhakikisha vijana wao wanabeba kombe hilo.
Mikakati iliyowekwa na timu hizo ndiyo itakayofanya hatua hiyo kuwa na upinzani mkali kwani malengo ya kila klabu ni kudhihirisha ubora kwa mpinzani wake na kupata nafasi ya kusonga mbele ili kuiwakilisha nchi kimataifa. Lakini mbali na mchezo huo kati ya Prisons na Simba, timu ya Mbao FC ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani imefanikiwa kupata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya wapinzani wao Polisi Tanzania katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Katika mchezo huo goli hilo la Mbao lilifungwa na mshambuliaji Waziri Junior dakika ya 65 lakini licha ya ushindi huo Mbao imeendelea kusalia nafasi ya 19 wakiwa na ponti 29.
Tanzania Prisons: Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya/Ismail Azizi dk61, Ezekia Mwashilindi, Samson Mbangula, Jeremiah Juma na Adil Buha.
Simba: Aishi Manula, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kennedyy Juma, Gerson Fraga, Hassan Dilunga/Luis Miquissone dk67, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/ Clatous Chama dk46 na Mraj Athumani ‘Madenge’/John Bocco dk 80.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464