STAND UNITED: WACHEZAJI 6 HAWAJARIPOTI KAMBINI MAANDALIZI YA FDL



Mwenyekiti wa Stand United, Dk. Ellyson Maeja

Na Sam Bahari - Shinyanga Press Club Blog
WAKATI ikijiandaa kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) tangu kurejea kwake kufuatia kusimama kwa ligi hiyo baada ya mlipuko wa ugonjwa COVID 19, timu ya Stand United ya mkoani Shinyanga imeeleza kuwa wachezaji wake sita hawajaripoti kambini kujiunga na wenzao kwa ajili ya michezo hiyo.

Stand United itashuka dimbani Juni 20, 2020 ugenini katika uwanja wa Ally Hasan Mwinyi mjini Tabora kuwavaa maafande wa Rhino Rangers kusaka alama tatu muhimu zitakazowapa matumaini ya kuendelea kusalia kwenye ligi hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Stand United, Dk. Ellyson Maeja amesema baada ya michezo kuruhusiwa na serikali mfadhili wa timu hiyo, kampuni ya vinywaji baridi Jambo Group Ltd aliamua kuwatumia wachezaji wote 27 nauli ya kurejea kambini.

Dk. Maeja amesema pamoja na wachezaji kutumiwa nauli na mfadhili lakini cha ajabu hadi leo Juni 17, 2020 ni wachezaji 21 ndiyo waliokwisha kuripoti kambini, huku wengine sita wakiwa hawajaonekana hadi sasa.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa wachezaji hao idadi na maeneo wanakotoka mchezaji mmoja kutoka wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, mwingine mkoa wa Kilimanjaro na Wachezaji wanne kutoka Jijini Dar es Salam.

“Hatujafahamu lengo la Wachezaji sita ambao hadi sasa hawajaripoti Kambini licha ya Mfadhili wetu wa Jambo Group Ltd kuwatumia fedha kwa ajili ya nauli,” amesema Dk. Maeja.

Akizungumza kwa njia ya Simu Kocha Mkuu wa Stand United, Atuga Manyundo amesema Vijana wako vizuri na kwa asilimia kubwa kurejea Ligi kuu Tanzania bara kwa musimu huu.

Kocha Manyundo alisema Timu ya Stand United inatarajia kumaliza Viporo vya kucheza na timu za Rhino Rangers Fc ya Tabora, AFC Arusha, Mawenzi Market Fc ya Morogoro na Sahare All Stars ya Tanga.












Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464