Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog
Kufuatia kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii nchini juu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumshikilia na kumhoji aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, taasisi hiyo imejitokeza na kukanusha uvumi huo ikieleza kuwa hawajawahi kumkamata wala kumhoji Kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Juni 30, 2020 na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge amewaonya wale wote wanaojaribu kutumia jina la taasisi kwa lengo la kuvuruga na kuzua taharuki kwa wananchi kuacha kufanya hivyo mara moja kwani iwapo watabainika watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Ruge ameeleza kuwa Takukuru inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na kwamba iwapo kuna jambo lolote la muhimu ambalo umma unapaswa kuelezwa taasisi hiyo huwa inafanya hivyo kwa kutumia njia sahihi za utoaji taarifa.
"Ofisi ya Takukuru mkoa wa Arusha inakanusha taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ikiwemo gazeti la Jamhuri la Juni 30-Julai 6, 2020, kuwa inamshikilia aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
"Taarifa hizi si za kweli kwani Takukuru mkoa wa Arusha haijawahi kumkamata wala kumhoji Mrisho Gambo," amesema Ruge.
Katika hatua nyingine, Ruge amewaasa wananchi na watu wote wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao, kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa kwani Takukuru mkoa wa Arusha inafuatilia nyendo zote za wote walioonesha nia ya kugombea na wapambe wao kuhakikisha kwamba hawatoi rushwa ili kuchaguliwa katika ngazi yoyote ile.