
Ujenzi wa eneo la lango (Water Intake) la kuingilia maji kwenda
kwenye mitambo ya kufua umeme katika Mradi wa Julius Nyerere (Mw 2115)
unatarajiwa kukamilika Februari, mwakani.
Msimamizi wa ujenzi wa njia za maji pamoja na bwawa kwenye Mradi wa
Julius Nyerere, Mhandisi Dismas Mbote, amesema jana utekelezaji wa njia
hiyo ulianza Oktoba, mwaka jana.
Ameongeza kuwa kazi ya uchimbaji wa lango imekamilika kwa kuchimbwa
kina cha mita 53 ambapo hivi sasa kazi inayoendelea ni uondoaji wa
kifusi na uchimbaji wa mahandaki matatu yatakayotumika kupitisha maji.

Aidha, amesema zitafanyika kazi za kuchoronga miamba pamoja na
kuimarisha kuta kwa zege. Maji yatakayofua umeme kabla ya kwenda kwenye
mitambo ya kufua umeme yataingia kwanza kwenye lango.
Pia amesema kwa hivi sasa imeletwa mashine ya kuchoronga miamba
ambayo ni ya kwanza kwa Tanzania na inayotarajiwa kuongeza kasi katika
uchimbaji wa mahandaki ya kupeleka maji kwenye mitambo.
Handaki la kwanza litakuwa na urefu wa mita 350, la pili mita 410 na la tano mita 570 hadi kwenye mitambo ya kufua umeme.
Chanzo: https://timesmajira.co.tz Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464