MAHAKAMA
ya Mkoa wa Lindi, imemuhukumu mkazi wa Kata ya Nyengedi, Kassimu Bidhali
Chilumba (18), kuchapwa viboko 12 makalioni, baada ya kupatikana na kosa la
kumbaka mwanafunzi.
Mtuhumiwa huyo alimbaka mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyengedi (jina limehifadhiwa).
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu wa Mahakama hiyo, Magala Muyonga, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, ambapo mshtakiwa alikiri kutenda kosa.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshtakiwa aliulizwa kama ana sababu zitakazoishawishi mahakama isimpe adhabu kali, kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza, ibirisi wa mapenzi ndiye aliyemshawishi kufanya yote hayo, hivyo anajutia, huku akiahidi kutorudia kosa.
Baada ya utetezi huo, Hakimu Muyonga alimuuliza mwanasheria wa serikali kama ana kumbukumbu ya makosa ya zamani ya mshtakiwa na kujibu hana, ingawa aliiomba Mahakama kumpatia mshtakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine wenye na tabia hiyo.
Hakimu Muyonga akitoa hukumu katika Shauri hilo namba 512020, kupitia vifungu vya sheria 130 (i) (2) (e) na 131 (2) (a) Sheria ya Elimu mwaka 2019, alisema amesikiliza maombi za pande zote mbili na kumuhukumu mshtakiwa Chilumba kuchapwa viboko 12 makalioni.
Awali ilidaiwa na Mwanasheria wa Serikali, Godfrey Mramba, kuwa mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu Juni 5, mwaka huu, majira ya alasiri.
Mramba alidai mtuhumiwa alikamatwa eneo ambalo kinajengwa choo kipya, kilichokuwa kinajengwa nyumbani kwa mzazi wa mtuhumiwa, wakati mwanafunzi huyo akiwa anapita eneo la nyumba hiyo.
CHANZO-IPPMEDIA Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464