VIWANJA VYA NANENANE SIMIYU KUWA KITUO CHA UENEZAJI TEKNOLOJIA

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi. Mtemi Msafiri aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima akifungua kikao cha maandalizi ya Maonesho ya Nanenane kitaifa mwaka 2020 ambayo yanafanyika kwa mara ya tatu mfululizo sasa katika kanda ya ziwa Mashariki viwanja vya Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu

Na Stella Kalinga, Simiyu RS.

Kituo cha utafiti wa kilimo nchini (TARI) kimechagua eneo la viwanja vya maonesho ya nane nane vilivyopo  kata ya  Nyakabindi wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kuwa kituo endelevu cha uenezaji wa teknolojia lengo likiwa kuwawezesha  wakulima kupata  huduma za kilimo kwa mwaka mzima.

Hayo yamebainishwa na Bibi. Mshaghuley Ishika kutoka TARI Dodoma kwenye kikao cha maandalizi nane nane kilichofanyika Juni 15, 2020 kwenye jengo la mkoa wa Simiyu lililopo kwenye viwanja hivyo kikwahusiaha viongozi wa Kanda ya ziwa Mashariki (Simiyu, Mara na Shinyanga).

Aidha, Ishika amesema kituo hicho kitawarahisishia wakulima kupata bidhaa zinazozalishwa kwenye Kituo hicho ambapo kwa hapa nchini huzalishwa katika vituo 17,  huku akibainisha kuwa TARI kwa kutambua hilo wameamua kuongeza eneo la vipando katika Viwanja vya Nyakabindi na kufikia hekari 3.

"Mbali na kuwa kituo endelevu cha usambazaji teknolojia kutakuwa vifaa na duka la mbegu zinazozalishwa na TARI  ambazo zinapatikana katika vituo 17 hapa nchini na  litamsaidia mkulima kujifunza mengi kuhusiana na kilimo; kituo hiki pia kimepatiwa mtumishi wa kudumu atakayekuwa anasambaza teknolojia kanda ya ziwa Mashariki ," amesema Ishika.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini  amesema maandalizi ya Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2020  yamefikia 70% na kuongeza kuwa kwa upande wa vipando vimefikia 75%.

Wakati huo huo  Sagini amewaomba  viongozi wote wanaotoka  kwenye mikoa inayounda kanda ya ziwa Mashariki (Simiyu, Mara na Shinyanga) wakiwemo wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji  kuhudhuria kikamilifu kwenye vikao vya maandalizi ili yale wanayokubaliana wayatekeleze kwa wakati.

Akizungumzia masuala  ambayo bado yanafanyiwa kazi Sagini amesema kwa sasa kamati ya maandalizi inaendelea na  ni ukarabati wa miundombinu ikiwemo   maji ,barabara na umeme huku akiwaomba washiriki kutoa michango yao mapema ili kufanikisha maandalizi kwa wakati.

Awali akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Mara,Mhe.Adam Malima, Mkuu  wa wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri ambaye pia  alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, ameuhakikishia umma kuwa Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 yatakuwa bora zaidi  na yataacha alama; kutokana na maonesho hayo  kufanyika kitaifa kwa miaka mitatu  mfululizo katika kanda ya ziwa Mashariki.

Katika hatua nyingine mhandisi Msafiri  amezitaka halmashauri zote ambazo hazijaanza na zile  ambazo maandalizi yake yanaenda taratibu, kuharakisha kusimamia maandalizi hayo na kuhakikisha yanakuwa ya kuridhisha, ili wakulima watakapokwenda kujifunza waone umuhimu wa kilimo chenye tija.


Kanda ya ziwa Mashariki inaundwa na mikoa mitatu ambayo ni Mara, Shinyanga na Simiyu na  mwenyeji wa maonesho ya Nane nane kitaifa ni mkoa wa Simiyu kwa miaka mitatu mfululizo sasa, ambapo  kwa mwaka 2020 kaulimbiu ya maonesho haya ni "KWA MAENDELEO YA KILIMO MIFUGO NA UVUVI CHAGUA VIONGOZI BORA 2020”
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464