Na Sumai Salum - Kishapu
Wanawake wajane wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wametakiwa kujipa moyo na kupata muda wa kutosha wa kupumzisha akili kabla hawajaamua kuingia kwenye mahusiano mengine mapya kwa lengo la kuondokana na changamoto na migogoro ya mahusiano baada ya kuwa wameondokewa na wenza wao.
Hayo yamesemwa leo Juni 23,2020 na Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Kishapu Bw. Joseph Swalala ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Wajane Duniani yenye kauli mbiu isemayo “HAKI NA ULINZI KWA WAJANE MSINGI IMARA KWA MAENDELEO YA JAMII” ambapo ameiasa jamii kutoendeleza mila na desturi kandamizi na zilizopitwa na wakati zenye lengo la kuwanyima wanawake wajane haki zao za umiliki mirathi pindi wanapofiwa na waume zao.
“Sheria ya mirathi inaeleza baada ya mme kufariki dunia mke anatakiwa awe msimamizi ila mila na desturi kandamizi zimekuwa zikipindisha sheria hii kwa kuchagua ndugu mme wa marehemu kuwa ndie msimamizi na mali zikishaisha anamterekeza , lakini pia niwashauri wanawake wajane wasiwahi kuolewa kwani wengi watakuja kwako kwa lengo la kufuja mali kisha wanaondoka ni heri utulie kwanza ujue nini cha kufanya ili kikusaidie wewe na watoto wako ulioachiwa”, aliongeza Swalala.
Pia Swalala alidai kuwa serikali inao utaratibu wa kutenga fedha aslimia 10 kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kuwaondolea liba tofauti na awali ambapo wanawake ni (4%) ,vijana(4%) na watu wenye ulemavu (2%) kwa lengo la kuwasidia kujiinua kiuchumi na kuongeza kipato huku akiziomba taasisi na mashirika binafsi kwa kujitoa kwa wingi ili kuwawezesha wajane.
Bi. Annastadhia Christopher Lwekila ambaye ni mjane anayeishi kijiji cha Isoso kitongoji cha Karume ambaye ni mama mwenye watoto 5 aliyekaa kwa miaka zaidi ya 6 bila mme wake na sasa anajishughulisha na ukulima na utengezaji mapambo ya ndani, amesema kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto za kutaka kurithiwa baada ya kufiwa na waume zao huku wajane wasio na watoto wakinyanyaswa na kufukuzwa kutokana na kuwa hawahesabiki katika familia ya upande wa mwanamme huku akitoa wito kwa wanawake kujishughulisha na biashara na kuondokana na utegemezi.
“Hali ya kunyanyaswa ipo kwa baadhi kwani siku ya matanga anachaguliwa mtu wa kuilinda familia na baadae anatumia zile mali vibaya na matokeo yake zikiisha basi anaondoka na kwa wajane ambao hawakubahatika kuzaa yaani hawana thamani kabisa na mshukuru Mungu sasa nina uwezo wa kujisimamia kiuchumi licha ya kuwa nina watoto wanaonitegemea sasa ni 2 kutokana na ukulima ninaoufanya pamoja na ususi za bidhaa mbalimbali za asili najipatia kipato mbali na kuwa sikuwa nikijishughulisha mme wangu kabla angali hai ila nawashauri jamii iwapende na kuwathamini wajane lakini pia wanawake wafanye kazi hata kama bado wanawaume zao maana kifo hakina hodi”, alisema Bi Lwekila.
Kivulini ni shirika linalotetea haki za wanawake na wasichana kwenye mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Shinyanga katika wilaya ya Kishapu ambapo Meneja miradi wa shirika hilo lisilokuwa la kiserikali Bi. Eunice Mayengela amesema kuwa uwepo wa siku ya wajane inawapa fursa ya kuendelea kuelimisha jamii juu ya haki sawa ya umiliki wa mali na kuwapa kipaumbele kwa kuwasaidia wajane kwa kutatua changamoto mbalimbali wanazopitia katika kipindi walipopoteza waume zao.
“Sisi kama shirika tuna haki ya kutetea wajane kwani imekuwa ni changamoto kubwa hususa ni kwenye jamii ya kisukuma mara nyingi tumekuwa tukiona baada ya kufariki mwanaume kunakuwa na migogoro huku mwanamke akifariki hakuna migogoro na hiyo ni kutokana na mila na desturi zinazoleta mitizamo mibaya na hata kunyanyaswa kingono wajane ili apate huduma kutoka kwa msimamizi wa familia kwani hawana elimu ya kutosha juu ya sheria ya mirathi ikiwamo muda wa kufungua shauri la mirathi kufunguliwa baada ya siku 90 kuwa ni nyingi na hawana elimuya kumsaidia piandi aonapo mali za marehemu zinatapanywa akaweke zuio mahakamani” ,alisema Bi. Mayengela.
Aidha Mayengela ameongeza kuwa ni wakati ambao jamii,watunga sera na watoa maamuzi kuweka nguvu za pamoja kwa kusimamia maswala ya upatikanaji haki za wajane kwa muda muafaka kwani mashauri mengi ya mirathi yamekuwa yakichukua miaka mitano hadi kumi kukamilika jambo ambalo kwa baaadhi ya jamii linalopelekea uvunjifu wa haki za wajane kwa kitopewa nafasi za kusimamia mali walizovuna pamoja na waume zao kiasi cha ndugu wa mwanaume kutapanya mali huku wajane na yatima wakihangaika kimaisha.
Bwana Habibu Makusanya ni mkazi wa Kishapu ambaye amelaani mila na desturi mbovu zinazo wanyima haki wanawake wajane ambao ndio wanatakiwa kuwa walithi wa mali hizo ambazo walikuwa wakikusanya na waume zao ili ziwasaidie wao na watoto waliochwa na baba wa familia huku akiwashauri wanaume kuwa na mazoea ya kuandika wosia kwani itaondoa utata wa kifamilia.
“Wito wangu ni kwa serikali ihakikishe inasimamia ulinzi wa wajane kwa sheria za nchi ili wapewe haki za usimamizi wa mali za urithi bila kuingiliwa na kubughuziwa na mtu yeyote,” Aliongeza Makusanya