Picha kwa hisani ya TimesMajira Online
Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog
Jumla ya
Wanachama 1,023,911 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mikoa yote 32 na
jumuiya zake zote wamemdhamini Rais Dk. John Magufuli ili aweze kugombea tena
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza
leo wakati wa kupokea fomu ya Rais Magufuli na fomu za wadhamini kutoka kwa
wenyeviti wa CCM katika mikoa yote 32 nchini na jumuiya zake, Katibu Mkuu wa
CCM Taifa, Dk. Bashiru Ally amesema kuwa amejihakikishia kuwa fomu aliyorejesha
Rais Magufuli imejazwa vizuri na Julai 10 Halmashauri kuu ya chama hicho itakaa
kumpigia kura awe mgombea wa chama hyicho kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka
huu.
Katika Udhamini
huo, Mkoa wa Morogoro umeongoza kwa kuwa na wadhamini wengi ambao ni 117, 450,
huku mkoa anaotoka Rais Magufuli, Geita akidhaminiwa na wanachama 89,595,
Kagera wakijitokeza 27,245, Kigoma 30, 220, Kilimanjaro 23,434 na Njombe
17,810.
Baadhi ya
mikoa mingine ni Shinyanga wadhamini 12,000, Katavi 5,700, Mtwara 7,566, Rukwa
5,600 na Simiyu 3,693.
Jumuiya ya
Wazazi ya chama hicho imemdhamini kwa wanachama 48,329, Jumuiya ya Vijana (UVCCM)
wadhamini 130,063 na Umoja wa Wanawake (UWT) wanachama 66,633, ambapo chama
hicho kimeazimia kushinda kwa asilimia 95 katika mikoa yote.
Kwa upande
wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Mohamed Shein binafsi
amemdhamini Rais Magufuli kwa wadhamini 800.
Katika hatua
nyingine, Dk. Bashiru amesema kuwa kuanzia kesho Julai 1, 2020 wanachama wa
chama hicho walio na nia ya kugombea nafasi za ubunge na udiwani waanze kupita kwenye ofisi za wakurugenzi wa
uchaguzi kuulizia utaratibu, ambapo ameweka wazi kuwa Julai 14 ndiyo siku ya
kuanza kuchukua fomu na zoezi litafungwa Julai 17, 2020 ambayo pia itakuwa siku
ya kurejesha fomu hizo.
“Tunahitaji
ushindani wa kistaarabu na tuna imani tutapata wagombea wazuri watakaokipatia
ushindi chama chetu,” amesema.
Rais
Magufuli
alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake kugombea nafasi ya Urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya pili Julai 11, 2020 na amerejesha
fomu hiyo leo Juni 30 na kuwashukuru wanachama kwa kuonyesha imani kubwa kwake.
Amewataka wagombea
wa nafasi za ubunge na udiwani kuwa wamoja na waache vitendo vya rushwa, na
pale atakapopatikana mwakilishi wa kupeperusha bendera ya chama hicho basi
aungwe mkono na umoja udumishwe.
Amesema amechukua fomu ili kuyaendeleza na kuyasimamia mambo mazuri ya kimaendeleo yanayofanyika nchini.