Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo
WANAFUNZI 73,101 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, ambapo kati yao wasichana 35,005 na wavulana ni 38,096.
Kwa upande wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu na elimu ya ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi ni 38,886, wakiwemo wasichana 14,510 na wavulana 24,376.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ualimu na vyuo vya elimu ya ufundi mwaka 2020 walitangazwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano wanatoka shule za Serikali, binafsi na waliosoma nje ya mfumo rasmi na waliosoma nje ya nchi baada ya matokeo yao kupata ulinganifu wa Baraza la Mtihani Tanzania.
“Idadi hii ni sawa na asilimia 93.4 ya wanafunzi wenye sifa za kuchukuliwa. Niwasihi wale wanaotaka kufanya mabadiliko ya kozi au chuo walichochaguliwa wasubiri hadi Agosti 1 mpaka 30 mwaka huu,”amesema Jafo
Aidha amesema katika kufanikisha adhima yao wanapaswa kuendelea kufanya bidii kwa kujifunza ili waweze kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu kidato cha sita na stashahada katika vyuo walivyopangiwa .
Pia aliwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano kuripoti rasmi kwenye shule walizopangiwa Julai 20, mwaka huu na kutahadharisha kwamba wale ambao hawataripoti wiki mbili tangu tarehe ya kufunguliwa shule nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii.
Katika hatua nyingine, Jafo aliwataka wakuu wa mikoa, makatibu tawala,wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhakikisha azima ya Serikali ya kila tarafa kuwa na shule ya kidato cha tano inatekelezwa ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.