Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (Wa nne kutoka kulia) akimtwisha ndoo yenye maji mmoja wa wakazi wa kijiji cha Uzogore wilayani humo wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji safi uliogharimu Sh Milioni 88, leo Juni 18, 2020.
Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mkoani humo, Jasinta Mboneko amewataka wakazi wa Kijiji cha Uzogore Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga kuilinda na kuithamini miundombinu ya maji iliyofikishwa katika makazi yao ili iwahudumie kwa muda mrefu zaidi na kwa malengo yaliyokusudia.
Mboneko ametoa kauli hiyo leo Juni 18, 2020 wakati akizundua mradi wa maji ya bomba kutoka Ziwa Viktoria utakaosadia kuondoa kero kwa wakazi hao waliokuwa wakifuata huduma hiyo umbali wa zaidi ya Kilomita 7 na kuhatarisha maisha yao hususan kwa wanawake na watoto.
DC Jasinta Mboneko akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa mradi huo.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo wa maji ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 ya kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma ya maji safi na salama sambamba na kumtua mama ndoo kichwani ili asisafiri umbali mrefu kuyasaka maji.
“Niwakumbushe tu jambo moja, lengo la Serikali ni kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani na kumondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta maji na kutohatarisha maisha yenu na watoto, kwa hiyo nina imani sasa mambo yatakuwa shwari,” amesema DC Jasinta.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Shinyanga, Emael Nkopi amesema kuwa mradi huo ulioanza kutekelezwa Februari 5, 2020 umegharimu Sh Milioni 88 zilizotokana na michango ya wananchi, RUWASA na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA).
Kaimu Meneja wa RUWASA Shinyanga, Emael Nkopi
Nkopi amebainisha kuwa RUWASA ilichangia Sh Milioni 50.4, SHUWASA Sh Milioni 31.7 pamoja na juhudi za wananchi waliojitolea kuchimba na kufukia ambapo thamani yake ni Sh Milioni 6.740.
“Mradi huu utawanufaisha wakazi zaidi ya 3,700 kutoka vitongoji sita vya kijiji cha Uzogore ambao wataondokana na changamoto ya kufuata maji umbali mrefu na watapata huduma hii kwa gharama nafuu,” amesema Nkopi.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA), Flaviana Kifizi amesema kuwa jukumu lao ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi, huku akiwataka wananchi kujiunga na huduma za maji nyumbani ili waweze kuyapata wakiwa majumbani mwao.
“Niwaombe wananchi hakikisheni mnaunganisha huduma hii majumbani kwenu ili muipate kwa ukaribu zaidi, unakuja kwetu tunakupigia hesabu tunakupatia baadae tunakuja kukuunganishia bomba la maji,” amesema Flaviana.
Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA), Flaviana Kifizi
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakiwemo Regina Mwabila, Zaituni Omary na Esther William wamemshukuru Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amabye alikuwa msitari wa mbele kuhakikisha maji hayo yanapatikana, kwani baada ya kusikia kilio chao na kufika katika kijiji hicho aliwahakikishia kuwa tatizo hilo litatatuliwa na sasa huduma hiyo imefika kama ilivyoahidiwa.
Katika hatua nyingine wakazi hao wameishukuru na kuipongeza Serikali ya awamu ya tano inayojali na kusikiliza kero za wanyonge kwa kuhakikisha kuwa wakazi hao wanapata huduma ya maji safi na salama ili kuwaepusha na magonjwa yaliyokuwa yakiwapata
Mwenyekiti wa Kijiji cha Uzogore, Peter Dotto amesema ujio wa maji hayo umesaidia kutatua changamoto hiyo ambapo wamekosa huduma ya maji safi na salama kwa zaidi ya miaka 30 ambayo ilichangia wakazi wengi kuugua magonjwa yaliyotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Uzogore, Peter Dotto
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na Meneja wa SHUWASA, Flaviana Kifizi wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Uzogore waliobeba ndoo za maji kichwani baada ya uzinduzi wa mradi wa maji safi kijijini hapo.
DC Jasinta Mboneko (katikati) pamoja na baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Uzogore.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (aliyevaa gauni la kitenge) akicheza ngoma na wananchi wa kijiji cha Uzogore manispaa ya Shinyanga wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji safi kijijini hapo.
Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliohudhuria uzinduzi huo
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na amani wilaya ya Shinyanga na watumishi wa SHUWASA wakifuatilia zoezi la mradi huo.
DC Mboneko akizindua rasmi huduma ya utoaji majisafi katika kijiji cha Uzogore
Wananchi wa kijiji cha Uzogole wakishuhudia uzinduzi huo
Baadhi ya wazee wa kijiji cha Uzogole nao walifika kushuhudia jinsi maji safi kutoka Ziwa Viktoria yanavyozinduliwa kijijini kwao.
Akina mama ambao ndiyo wahusika wakubwa wa changamoto ya upatikanaji wa maji, nao walifika kuona jinsi neema hiyo ilivyofika kijijini kwao na kuwapunguzia changamoto hiyo.
DC Mboneko akifurahia baada ya majisafi kutoka Ziwa Viktoria yakizinduliwa katika kijiji cha Uzogole manispaa ya Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464