WAZIRI ASHTUSHWA MATUMIZI MAKUBWA YA BANGI NCHINI, NDANI YA MIAKA 5 KILO 188,489.93 ZAKAMATWA


Bangi
SERIKALI imesema bado kuna tatizo la matumizi makubwa ya bangi nchini ambapo mwaka 2015 hadi Juni, 2020, kilo 188,489.93 za bangi zimekamatwa.

Hayo yalielezwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana, Sera na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika siku ya maadhimisho ya kupinga vita dawa za kulevya duniani.

Jenista alisema bado tatizo la matumizi ya bangi ni kubwa nchini ambapo Serikali inajitahidi kulitatua na kwamba wamefanikiwa kukamata kilo 124,080.33 za mirungi kilo 58.46 za Cocaine na kilo 635.57 za heroin.

Alisema katika ukamataji huo, watuhumiwa 73,920 walikamatwaa ambapo pia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imefanikiwa kufanya ukaguzi katika makampuni 167 yanayojihusisha na uingizaji wa kemikali bashirifu.

Alisema katika ukaguzi huo, mamlaka imefanikiwa kukamata kiasi lita za ujazo 480,000 na kilo 22,145 za kemikali bashirifu zilizoingia nchini bila ya kufuata utaratibu.

Alisema tatizo la dawa za kulevya katika jamii ni mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta mbalimbali katika kupambana nalo.

Alisema DCEA inatekeleza majukumu yake ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kwa kushirikiana na wizara mbalimbali, vyombo vya ulinzi na usalama, na taasisi zingine za Serikali na zisizo za Serikali pamoja na mashirika ya kitaifa na kimataifa.

Alisema mwaka 2015-2020, mamlaka imetekeleza kazi mbalimbali katika kukabiliana na dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2017.

Pia imetoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya ambapo mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu imeweza kuanzisha vilabu vya kupinga dawa za kulevya mashuleni.

“Vile vile, elimu bora kuhusu tatizo la dawa za kulevya imekuwa ikitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama vile televisheni, magazeti, warsha za kitaifa na makongamano pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu madhara ya dawa hizo pamoja na udhibiti wa uchepushwaji wa kemikali bashirifu.

“Hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia wimbi la vijana kuingia kwenye matumizi na biashara ya dawa hizo,” alisema.

Alisema pia imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhoofisha na kuvunja mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

Waziri Jenista alisema kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2019 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa 90%.

Pia, mamlaka imeshinda kesi kubwa za wafanya biashara wakubwa wa dawa za kulevya.

“Upanuzi wa huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na taasisi zingine zisizo za kiserikali imefanikiwa kupanua huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini, ambapo hadi mwaka 2016 kulikuwa na vituo vitatu tu nchini ambavyo vilihudumia waathirika 3,500.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464