Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum (CCM) akirejesha fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo leo Julai 14, 2020 masaa mawili baada ya kuichukua.
Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
JUMLA ya wagombea 24 wakiwemo wanawake wawili wamechukua
fomu za kuwania ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga kwa tiketi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya zoezi la uchukauji fomu ndani ya chama
hicho kufunguliwa leo Julai 14, 2020, huku 13 wakichukua katika jimbo la Solwa
mkoani humo, ambapo Mbunge anayetetea kiti chake, Ahmed Salum akirejesha fomu
baada ya masaa mawili.
Miongoni mwa waliochukua fomu katika jimbo la Shinyanga
mjini hii leo ni Jeolojia Eunice Jackson na Mwenyekiti wa Chemba ya
Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Shinyanga, Dk. Kulwa Meshack.
Wengine ni Mkurugenzi wa asasi ya Kiraia TVMC, Mussa Ngangala, Mwanasheria wa kujitegemea,
Hassan Fatiu, Mfanyabiashara, Bandora Milambo, Grace Antony Lyon na John
Mlyambate.
Akizungumzia mchakato huo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM
Shinyanga Mjini, Said Bwanga amesema mchakato unaendelea vizuri na unaonyesha
kwamba wanachama wana msisimko wa kutaka kugombea, pia hali ni shwari na
wagombea wameelimishwa kutoshindana wao kwa wao kwa kufanyiana vurugu.
“Tumezuia maandamano wakati wa kuja kuchukua fomu,
tunaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kunakuwa
na amani wakati huu wa mchakato wa uchukuaji fomu na mgombea yeyote atakayehusika
kwenye vitendo vya rushwa chama hakitosita kumchukulia hatua," amesema.
Kwa upande wa jimbo la Solwa, mbunge anayetetea kiti chake,
Ahmed Salum alichukua fomu saa 2 asubuhi na kuirejesha saa 4 asubuhi katika
ofisi ya chama hicho, ambapo wanachama wengine waliojitokeza kuchukua fomu ya
ubunge ni Mhadhiri wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Christian Misobi.
Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Salum amesema
anawashukuru viongozi wa chama hicho kwa kutengeneza mfumo mzuri wa
kidemokrasia katika kupata wagombea ambao unatoa demokrasia ndani ya chama.
“Kikubwa tuchukue fomu tujaze tumtangulize Mungu, tusubiri
mchakato ndani ya chama endapo jina langu likipendekezwa kama mgombea wa CCM
ndipo nitazungumza zaidi,” amesema.
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini (Jimbo la Solwa),
Erenestina Richard amesema wagombea 13 wamejitokeza baada ya zoezi hilo
kufunguliwa hadi muda wa saa 4 asubuhi, ambapo ameeleza kuwa wanaamini kadri
muda unavyokwenda watazidi kujitokeza wanachama wengi wenye nia ya kuchukua
fomu, huku maelekezo ya chama yakifuatwa na wagombea hao.
Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Erestina Richard akimkabidhi fomu ya ubunge, Christian Misobi anayewania ubunge wa Jimbo la Solwa
Ahmed Salum akisalimiana na baadhi ya wanawake waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania udiwani (Viti maalum) jimbo la Solwa.
Jeolojia Eunice Jackson Wiswa akionyesha fomu yake ya kuwania ubunge jimbo la Shinyanga Mjini
Afisa Uhusiano halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, John Mlyambate akionyesha fomu ya kuwania ubunge jimbo la Shinyanga mjini.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Shinyanga, Kulwa Meshack akionyesha fomu ya kuwania ubunge jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya CCM baada kuchukua fomu leo.