Ahmed Salum
Na Damian Masyenene –Shinyanga Press Club Blog
Baada ya ushindi wa kura 377 za maoni dhidi ya 304 za
mpinzani wake wa karibu kwenye kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuteuliwa kugombea ubunge wa Jimbo la Solwa (Shinyanga
Vijijini) mkoani Shinyanga, Ahmed Salum amesema sasa anasamehe vitendo vyote
alivyofanyiwa wakati wa mchakato huo na ameamua kusonga mbele, huku akijinasibu
kuwa uwezo wa kupmbana na wagombea wa vyama vya upinzani anao.
Ahmed ambaye ni mgombea anayetetea kiti cha ubunge wa jimbo
hilo baada ya kuliongoza kwa miaka 15, ametoa kauli hiyo leo Julai 20, 2020
kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga wakati akitoa neno la shukrani
kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Vijijini baada ya kutangazwa
kuwa mshindi wa kura za maoni.
Mwanasiasa huyo amesema kuwa endapo jina lake litateuliwa na
CCM basi anaahidi ushirikiano kwani hana kinyongo japokuwa anafahamu vita
ilikuwa kubwa sana, ambapo amewaomba wana CCM wote wakiwemo watia nia wenzake
kuvunja makambi (makundi) na kusonga mbele kwa manufaa ya chama hicho.
“Sina kinyongo, nafahamu vita ilikuwa kubwa sana lakini
naomba tuvunje makundi nimesamehe yote na kwa yeyote aliyenikwaza nimemsaheme….uwezo
wa kupambana na wagombea wa upinzani ninao kwahiyo tuendelee kushirkiana,”
amesema.
Naye mshindi wa pili katika kura hizo za maoni, Azza Hilal
amesema kuwa wajumbe (wapiga kura) wametenda kile kilichostahili kwa kila
mgombea, hivyo akawaomba wagombea wenzake kusonga mbele na kuyazika yale yote
yalitokea nyuma.
“Niwaombe wagombea wenzangu hili limekwisha hakuna cha ‘Team
Azzah’ ama nani bali hii ni timu CCM, nawashukuru kwa kura mlizonipa hii ni
heshima kwangu,” amesema Azza.
Akitoa neno kwa niaba ya watia nia wengine 52, Mzee Sprian
Mnyedu amewapongeza wenzake kwa uvumilivu mkubwa waliounyesha na kuhakikisha
zoezi hilo linamalizika salama, na kuwataka wenzake kuungana ili Solwa isonge
mbele na kupiga hatua za maendeleo.
“Nashukuru Mungu kwa zoezi hili kumalizika salama bila
mihemko, tukubali kwamba mambo yameisha na tuwe marafiki, aliyeshinda
tunampongeza kile alichokipata ni maamuzi ya wanachama na tunakiheshimu,”
amesema.