Ahmed Salum akizungumza wakati wa kujinadi kabla ya zoezi la upigaji kura
Na Damian Masyenene -Shinyanga Press Club Blog
JITIHADA za Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ahmed Salum
kutetea kiti cha Ubunge wa Jimbo la Solwa mkoani Shinyanga zinazidi kuzaa
matunda baada ya hii leo kushinda kura za maoni jimboni humo.
Ahmed Salum ameliongoza Jimbo la Solwa kwa muda wa miaka 15 (2005-2020).
Zoezi la upigaji kura za maoni kwa watia nia wa ubunge jimbo
la Solwa lilianza leo Julai 20, 2020 katika Uwanja wa CCM Kambarage, mjini
Shinyanga majira ya saa 8 mchana (watia nia kujieleza) na saa 12 jioni zoezi la
kuhesabu kura likaanza hadi saa 2 usiku.
Ambapo jumla ya watia 54 waliomba ridhaa ya CCM kuwateua ili
wagombee ubunge jimboni humo, huku ushindani ukiwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Viti
Maalum Mkoa wa Shinyanga, Azzah Hilal Hamad (CCM) na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo
hilo, Ahmed Salum.
Azzah Hilal akizungumza mapema kabla ya zoezi la upigaji kura
Kwa Mujibu wa Msimamizi Mkuu wa zoezi hilo, Peter Gawiza
ambaye ni Mjumbe Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Mwenyekiti
wa Wazazi CCM wilayani humo, wajumbe waliotakiwa kuhudhuria uchaguzi huo ni
843, waliohudhuria ni 834, waliopiga kura ni 823, kura zilizoharibika ni 0 na
kura halali ni 823.
Gawiza alimtangaza Ahmed Salum mshindi wa kura hizo baada ya
kupata kura 377 dhidi ya 304 za mpinzani wake wa karibu, Azzah Hilal, huku Jeremiah
Jilili akiibuka mshindi wa tatu kwa kura 35, Sosthenes Katwale kura 21, SPA
Mussa Singu (20) na Amos Mshandete kura 12.
Kwa mujibu wa Gawiza, watia nia 25 hawakupata kura hata
moja, 10 walipata kura moja kila mmoja, sita wakapata kura mbili kila mmoja,
wawili wakaambulia kura tatu tatu, wawili wakapata nne kila mmoja na wawili
wengine wakaambulia kura tano kila mmoja.
Akitoa neno kwa wagombea, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga,
Jasinta Mboneko amewapongeza watia nia wote waliogombea, huku akisistiza kwamba
kinachoshinda ni chama (CCM) na siyo mtu, hivyo amewataka wote kuhakikisha
chama hicho kinaibuka na ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao na pia wagombea
kufanya kampeni za kistaarabu.