AJALI YAUA WATATU DODOMA WAKIELEKEA MKUTANO MKUU CCM, YUMO DAS WA HANDENI

Magari mawili yamegongana uso kwa uso usiku wa kuamkia jana katika eneo la Vikonje mkoani Dodoma na kuua watu watatu, akiwemo Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Boniface Maiga Wengine waliofariki kwenye ajali hiyo ni dereva na kondakta wa basi.

Taarifa za awali zilidai kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 7 usiku baada ya gari la Mbunge wa Handeni, Omari Kigoda kugongana na basi aina ya Tata. Kigoda anadaiwa kuvunjika vidole viwili vya mkono wa kulia. Gari hilo la Kigoda lilikuwa na watu wanne ambao ni Kigoda, Maiga (DAS), dereva na msaidizi wa Kigoda.

Walikuwa wakienda Dodoma kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alithibisha kutokea kwa ajali hiyo.
Alipohojiwa kuhusu majina ya watu wengine waliokufa, alisema yuko mkutanoni na atatoa taarifa baadae. Dereva wa gari la Kigo- da, Peter Mganga alisema chanzo cha ajali hiyo, kilitokana na mwendo kasi wa dereva wa basi.

Alisema DAS alipoteza maisha hapo hapo huku wao wakikimbizwa katika Hospitali ya Chamwino kwa ajili ya matibabu. Alisema Kigoda alifanyiwa upasuaji wa vidole hivyo na baadaye waliamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, maarufu kama General.

Dereva huyo alisema baada ya kupata mati- babu, wawili waliruhusiwa kutoka hospitalini hapo saa 11:00 alfajiri. Alisema Kigoda alibaki kuendelea na matibabu ya vidole alivyoumia.

Alisema katika gari hiyo ya Kigoda walikuwa yeye, Kigoda, Mbelwa Saidy ambaye ni ndugu yao na Maiga (DAS). Alisema kuwa mwili wa marehemu upo hospitali hiyo ya mkoa wa Dodoma.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464