Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji (kushoto) akikaribishwa ndani ya CCM na Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.
Mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
katika Jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam umemalizika saa 10 jioni kwa kada wa
chama hicho, Furaha Dominic Jacob kuibuka kinara kwa kupata kura 101.
Furaha aliwashinda washindani wake wengine waliomfuatia kwa
karibu ambao ni Angella Charles Kiziga (85) na Mchungaji Josephat Gwajima
aliyepata kura 79 katika nafasi ya tatu.
Hata hivyo jimbo hilo lilikuwa na msururu mrefu wa majina ya
wanasiasa vijana mashuhuri na viongozi mbalimbali ambao wameshindwa kufua damu.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent
Mashinji aliyeambulia kura 2, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba
aliyepata kura tatu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi (MCL), Francis Nanai
aliyepata kura 5, huku aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta
naye akipata kura 61.