ASKOFU MBOTTO: RAIS MAGUFULI AMETUHESHIMISHA, NI KAMA MFALME DAUDI


Askofu Msaidizi wa Jimbo la Misungwi Kanisa la EAGT Bonde la Baraka, Onesmo Mbotto

Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog

MAAMUZI ya busara yaliyofanywa na Serikali chini ya usimamizi uliotukuka wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona yameendelea kuwagusa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, ambao wanasifu na kushukuru uamuzi wa kutofungia ibada na misa.

Mmoja wa walioguswa na jambo hilo na kutoa pongezi zake kwa Serikali ni Askofu Msaidizi wa Jimbo la Misungwi Kanisa la EAGT Bonde la Baraka, Onesmo Mbotto ambaye amesema kwamba Rais Magufuli ni zaidi ya Mfalme Daudi kwani anashindana na pepo wabaya wanaotaka kuiharibu nchi ya Tanzania.

Askofu Mbotto ametoa pongezi hizo Julai 5, 2020 mjini Misungwi wakati akizungumza na waumini wa kanisa hilo kwenye ibada ya Jumapili, ambapo akinukuu maandiko matakatifu katika kitabu cha Yeremia 32:27, Waebrania 12:28-29 na Wafilipi 2:8-9 ameeleza kuwa Tanzania imemtegemea Mungu na ina hofu ya Mungu ndiyo maana watumishi na watendaji wa serikali wamedumisha nidhamu sehemu za kazi kutokana na usimamizi madhubuti wa Rais Magufuli.

“Kwa sababu hiyo mpaka hapa tulipo tunakubalika na tunaheshimika kimataifa, ujinga, umaskini, ujambazi wa kutisha na mauaji vimekomeshwa na kuangushwa na tumeona usimamizi mzuri katika sekta ya madini, kwahiyo kwa mujibu wa kitabu cha Warumi 13:1 mamlaka ya Rais wetu imeamliwa na Mungu na tunapaswa kuyatii,” amesema.

Akizungumzia kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, Askofu Mbotto amesema viongozi wanaomaliza muda wao wamefanya mambo makubwa, hivyo wananchi wawe makini na wasifanye makosa katika kupata viongozi wapya, huku akiwataka kuchagua viongozi waadilifu, waaminifu na wachapakazi watakaotatua kero za wananchi.

“Tumevuka salama mpaka hatua hii kwa sababu ya utukufu na neema ya Mungu, Serikali yetu iendelee na imani na msimamo huu wa kuheshimu uwepo wa Mungu ili tuzidi kubarikiwa na tusitumbukie kwenye mitego ya shetani,” amesema.

Mmoja wa wazee wa kanisa hilo, Leonard Mosha ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo kanisani hapo, amesema kuelekea uchaguzi mkuu wanahitaji viongozi wenye moyo wa kujituma, kujitoa, wapenda haki na maendeleo na wasioendekeza rushwa.

“Viongozi wanaomaliza muda wao wamefanya kazi kubwa hasa Rais Magufuli na wasaidizi wake, tunahitaji viongozi watakaokuja wawe na nguvu na kumsaidia zaidi azidi kusonga mbele,” amesema.

Shemasi wa kanisa hilo, Joyce Masawe amesema kupitia nafasi ya mama ndani ya kanisa wanawahamasisha akina mama kuwa sehemu ya kuleta maendeleo kwa kukataa rushwa na kupata viongozi na wasimamizi sahihi wa rasilimali za nchi, huku akiwahimiza wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi.

“Nawatakia pia akinamama watakaojitokeza kwenye uchaguzi huu washinde kwa kishindo pia tunahitaji kiongozi mwenye hofu ya Mungu kama ilivyo kwa Rais Magufuli,” amesema.

Martha Onesmo ambaye ni Mkurugenzi wa umoja wa wanawake wa injili (WWI) Jimbo la Misungwi, amesema wanawake ni jeshi kubwa katika maombi ambapo kila mara wanaliombea taifa lipite salama katika kipindi cha uchaguzi.

Naye Katibu wa vijana kanisani hapo na kiongozi wa kusifu na kuabudu, Joseph Nyoni amewahimiza vijana wenzake kutohusika kwenye vitendo vya vurugu vitakavyoondoa amani wakati wa kampeni za uchaguzi, huku pia akiwasihi kujitokeza kwenye shughuli za maendeleo, kugombea na kupiga kura.
 
Waumini wa kanisa hilo wakifurahia neno la Mungu
  Askofu Msaidizi wa Kanisa la EAGT Jimbo la Misungwi Bonde la Baraka, Onesmo Mbotto akitoa mahubiri kwa waumini wa kanisa hilo.
Baadhi ya Wazee wa kanisa hilo
Waumini wa kanisa hilo wakifuatilia mahubiri kwa umakini mkubwa
Sehemu ya kwaya ya kanisa hilo ikitimiza wajibu wake
Waumini wakishiriki ibada
Wanakwaya wakiendelea kumuimbia Mwenyezi Mungu
Waumini wa kanisa hilo wakisikiliza neno la Mungu
Kwaya ya akina mama ikiburudisha
Mama Mchungaji, Martha Onesmo akiomba na kumshukuru Mungu
Wanakwaya wakimsifu Mungu kwa nyimbo mbalimbali
Wazee wa kanisa hilo wakifuatilia ibada
 Askofu Msaidizi wa kanisa hilo, Onesmo Mbotto
Mama Mchungaji, Martha Onesmo pamoja na Askofu Msaidizi wa kanisa hilo, Onesmo Mbotto
 Waumini wakifuatilia neno la Mungu
 Wanakwaya wakiomba na kusali
 Waumini wakiimba na kusifu







Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464