JESHI la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia Doria Frank (55) mkazi wa Kata ya Mamba Kaskazini Wilaya ya Moshi kwa tuhuma za kumchoma mjukuu wake.
Akizungumza na wanahabari mjini Moshi, Kamanda wa Polisi mkoani hapo Emmanuel Lukula, alisema tukio hilo lilitokea Julai 10 mwaka huu Saa 11:00 asubuhi huko maeneo ya Mamba Kata ya Mamba Kaskazini.
Alisema katika tukio hilo, mtoto mwenye umri miaka sita mwanafunzi wa shule ya awali St. Paul Albert aliuguzwa moto kuanzia chini ya kitovu hadi maeneo ya miguuni juu ya magoti na bibi yake mzaa baba aitwaye Doria Frank (55) mkulima mkazi wa Mamba.
Kamanda alisema kuwa, wakati mtoto huyo akiendelea kuungua na moto huo, majirani walisikia kelele za vilio na kujitokeza kwa ajili ya kutoa msaada ambapo walifanikiwa kuuzima moto kwenye mwili wa mtoto huyo.
“Moto huo tayari ulishamjeruhi vibaya mwili wa mtoto huyo,hali iliyompelekea maumivu makali,” alisema .
Alisema mtuhumiwa wa tukio hilo amekamatwa na jeshi hilo na majeruhi amehamishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi kwa matibabu zaidi akitokea hospitali ya Marangu alipokuwa akipatiwa matibabu ya awali.