Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magaharibi, Said Pamui akimkabidhi Meza Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Matha Mkupas kama ishara ya kukabidhi madawati 153.
Na Salvatory Ntandu - Mbogwe
Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita inakabiliwa na uhaba wa viti
na meza 1942 katika shule zake za sekondari 16 zenye jumla ya wanafunzi 8,975, hali inayosababisha baadhi yao kusoma
kwa awamu ili kukabiliana na tatizo hilo.
Kauli hiyo imetolewa Jana Julai 6, 2020 na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,
Elias Kayandabila katika hafla ya kupokea
viti na meza 153 vilivyotolewa na Benki ya CRDB katika shule ya Sekondari
Masumbwe ili kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema kuwa shule hiyo inahudumia kata tatu zilizopo karibu na kata
ya Masumbwe ikiwemo Nyakafulu yenye idadi kubwa ya wakazi
kutokana na shughuli za uchimbaji ambapo kwa sasa ina viti na meza 1007 na
upungufu ni 825 ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi ambao ni 1832 sawa na
asilimia 45.
“Baada ya Serikali kuanza kutoa elimu msingi bure idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa wingi kutokana na jamii za wafugaji kuwa
na mwamko wa kuwapeleka watoto shule,” alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya CRDB Kanda
ya Magaharibi, Said Pamui alisema kuwa msaada wa viti na meza walivyotoa vimegharimu Sh Milioni 9,945,000, huku akiwataka
wanafunzi kuyatunza ili yaweze kuleta tija sambamba na kupunguza tatizo hilo.
“Nitoe rai kwa wadau wengine nchini
kuiga mfano wa CRDB kwa kutoa misaada ya elimu katika halmashauri hii ili
kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea maendeleo
wananchi wake kwa kuwapatia huduma nzuri na stahiki,” alisema Pamui.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Matha Mkupas alisema kuwa uhitaji wa viti, meza na
madawati katika shule za msingi na sekondari bado ni mkubwa na kuwaomba wadau na
wazazi kushirikiana na serikali ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi
wa haraka, huku akiishukuru CRDB kwa kuiunga mkono serikali katika nyanja mbalimbali
ikiwemo elimu.
“CRDB ni benki ya kizalendo imekuwa
ikitushika mkono katika shughuli mbalimbali za kitaifa tunazozitekeleza katika
wilaya hii, niwasihi wananchi, wajasiriamali na watumishi wetu waendelee kuitumia na sisi kama serikali
tutahakikisha tunakuwa pamoja,” alisema Mkupasi.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya
Magaharibi, Said Pamui akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Mbogwe, Matha
Mkupas, Mkurugezi wa Halmashauri ya Mbogwe, Elias Kayandabila na baadhi ya
wanafunzi wa shule ya sekondari Masumbwe baada ya kukabidhi msaada wa viti na meza shuleni hapo.