Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya
Mussa Said akimkabidhi Kuku mmoja wa wahanga wa utelekezaji Wilaya ya Wete ikiwa ni miongoni mwa juhudi za TAMWA Zanzibar
kuwawezesha wanawake hao kujisimamia kiuchumi.
Na Gaspary Charles- TAMWA Zanzibar
FAMILIA za waathirika wa vitendo vya udhalilishaji kisiwani
Pemba wameshukuru na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar za kupambana na vitendo vya
udhalilishaji katika jamii.
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya
wanafamilia hao mara baada ya kukabidhiwa Kuku na chama hicho kwaaajili ya
uguaji ikiwa ni sehemu ya juhudi za chama hicho kupambana na vitendo vya udhalilishaji.
Mmoja wa wanufaika wa msaada huo Bi Mpemba Ali Moh’d amesema
Kuku hao watawasaidia kujiendeleza kiuchumi kulingana na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana
nayo.
“Tunawashukuru sana watu wa TAMWA kwa kutambua matatizo yetu
na kuamua kutuletea msaada huu wa Kuku kama sehemu ya faraja kwetu, tunajisikia
furaha sana kwakweli leo,” alisema.
Aidha ameongeza kuwa kutokana na familia hizo kuwa katika
hali ngumu ya maisha kupitia ufugaji wa Kuku itawawezesha kurahisisha
upatikanaji wa huduma za msingi katika familia zao.
“Kupitia Kuku hawa tuliopewa leo watatusaidia sana
kututalulia shida nyingi majumbani mwetu kama vile chakula kulingana na hali
zetu ndio kama hivo hatujiwezi na hatuna shughuli nyingine yoyote ya kutupatia kipato,”
alisema Mpemba.
Kwa upande wake Shaali Makame Sahaali amesema licha ya Kuku
hao kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi lakini pia imechochea hamasa kwa familia
hizo kujiona kuwa sehemu ya jamii kulingana na hali zao.
“Niseme tu kwamba TAMWA imefanya jambo kubwa sana leo kwani
licha ya mitihani tuliyokumbana nayo lakini kupitia hili nasisi tumefarijika
sana na kujiona kuwa sehemu ya jamii,” alisema.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, katibu wa Sheha ya Kiwani
Wilaya ya Mkoani, Mohamed Haji Suleiman alishukuru mchango wa TAMWA Zanzibar katika
kulinda na kutetea haki za kijamii Zanzibar na kukitaka chama hicho kuendelea
na juhudi hizo ili kuhakikisha jamii inabaki salama.
“Juhudi hizi zinazoendelea kuchukuliwa na TAMWA si kazi
ndogo. Niwaombe sana endeleeni na juhudi hizi ili kuhakikisha mnasaidia kutokomeza
vitendo vyote vya udhalilishaji katika jamii zetu Zanzibar,” alisema.
Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya
Mussa Said amesema lengo la kutoa msaada wa Kuku kwa familia za wahanga wa
vitendo vya udhalilishaji ni kuwawezesha kuwa na shughuli za kujiingiza kipato katika
familia.
“Tumeamua kutoa msaada huu kwa familia hizi ili uwasaidie kuendeshwa
familia zao kutokana na wengi wao kuwa katika hali ngumu ya maisha,” alisema.
Aidha mratibu huyo ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya
utekelezaji wa mradi wa kupinga udhalilishaji Zanzibar katika kuwawezesha
wahanga kujihusisha na shughuli za uzalishaji ili kuwa na uwezo wa kufuatilia kesi
zao mahakamani.
Alisema, “miongoni mwa malengo ya kutolewa kwa Kuku hawa ni
kuwawezesha kupata shughuli ambayo itawasaidia kupata kipato cha kufuatilia kesi
zenu ili muweze kupata haki zenu.”
Jumla ya Kuku 300 wamegawiwa kwa familia 30 za wahanga wa
vitendo hivyo kutoka Wilaya ya Mkoani na Wete Pemba.
Afisa Masoko kutoka Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake
TAMWA Zanzibar, Muhidin Ramadhan akimkabidhi Kuku mmoja wa
wahanga wa Utelekezaji Wilaya ya Mkoani.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya
Mussa Said akikabidhi Kuku kwa familia za wahanga wa vitendo vya
udhalilishaji katika Ofisi za TAMWA Pemba.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya
Pemba, Fat-hiya Mussa Said akimkabidhi Kuku Mpemba Ali Moh’d wakati wa zoezi la
Utoaji wa Kuku kwa wahanga wa Utelekezwaji Wilaya ya Mkoani Pemba.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya
Mussa Said akikabidhi chakula cha Kuku kwa mmoja wa wahanga wa Utelekezaji mara
baada ya kukabidhiwa Kuku mapema leo Julai 22 huko Ofisi za TAMWA Pemba.