HALMASHAURI YA USHETU YAITIMIZIA AHADI SHINYANGA SUPER QUEENS

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal alipoizindua rasmi timu ya wasichana ya Shinyanga Super Queens mnamo Machi 8, 2020 katika eneo la Iselamagazi halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Na Mwandishi Wetu - Shinyanga Press Club Blog
IKIWA ni takribani miezi minne imepita tangu kuzinduliwa rasmi kwa timu ya soka ya wanawake ya mkoa wa Shinyanga, Shinyanga Super Queens mnamo Machi 8, 2020 na kuahidiwa mambo kemkem kwa ajili ya kutimiza mahitaji yake, hatimaye Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama imetimiza ahadi iliyoahidi.

Shinyanga Super Queens ilizinduliwa Machi 8, 2020 kwenye uwanja wa Iselaghazi na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal (CCM) wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani, ambapo Mbunge huyo aliipatia jezi seti moja na mpira mmoja, huku Sh 280,000, mipira saba na jezi seti moja zikiahidiwa na wakurugenzi wa halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga. 

Ambapo miongoni mwa ahadi zilizotolewa ni kutoka Halmashauri ya Ushetu walioahidi Sh 200,000 ambazo zimekabidhiwa jana Julai 9, 2020 na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Verena Ntulo aliyemkabidhi Mkurugenzi wa timu hiyo, Flora Gaguti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya timu.

Akizungumza na Shinyanga Press Club Blog, Mkurugenzi wa Shinyanga Super Queens, Flora Gaguti ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono, ambapo halmashauri hiyo imeweza kutambua vipaji vya vijana wa kike katika mkoa wa Shinyanga.

Amesema kwa kuwa timu yake inajiandaa kushiriki michuano ya Ligi daraja la kwanza ili kupata nafasi ya kucheza ligi kuu ya wanawake nchini,  bado wanayo mapungufu makubwa kwani hawajapata vifaa vya michezo vya kutosha kwa ajili ya maandalizi ya ligi zinazokuja.

   "Tunaomba 'support' kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuweza kuwatia nguvu vijana wa kike kuendeleza vipaji vyao na kujipatia ajira ili kupunguza utegemezi na mimba za utotoni katika mkoa wetu wa Shinyanga," amesema Flora.
Kikosi cha Shinyanga Super Queens
 Furaha baada ya timu hiyo kuzinduliwa

Picha kwa hisani ya Malunde 1 Blog




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464