Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (wa pili kutoka kulia) akipokea hundi ya Sh Bilioni 1.5 kutoka Twiga Minerals Corporation Ltd zilizokabidhiwa na Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu (kushoto). katikati ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba na kulia ni Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila.
Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
Halmashauri za Mji wa Kahama na Msalala zimekabidhiwa hundi zenye thamani ya Sh Bilioni 1,535,821,894.85 kama malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia Januari hadi Juni, 2020 kutoka Kampuni ya Uchimbaji madini ya Twiga Minerals kupitia migodi yake ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu.
Ambapo Mgodi wa Buzwagi umelipa Sh Bilioni 1,159,817,107.83 kwa halmashauri ya Mji wa Kahama, huku mgodi wa Bulyanhulu ukilipa Sh Milioni 376,004,787.02 kwa halmashauri ya Msalala.
Malipo hayo yanafanyika ili kutekeleza hitaji la kisheria lakini pia ikiwa ni sehemu ya mikataba ya makubaliano kati ya migodi hiyo miwili na halmashauri husika ambayo inalenga kuboresha utoaji wa huduma katika jamii zinazozunguka migodi hiyo katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya na upatikanaji wa maji safi na salama.
Zoezi la kukabidhi hundi hizo limefanyika leo Julai 15, 2020 mjini Kahama
katika ofisi za Halmashauri ya Mji wa Kahama likihudhuriwa na Mkuu wa wilaya
hiyo, Annamringi Macha, Mkurugenzi wa Mji wa Kahama, Anderson Msumba pamoja na
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya hiyo, Joachim Simbila.
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha
Akipokea hundi hizo, Mkuu wa Wilaya ya
Kahama, Anamringi Macha amesema malipo hayo ya ushuru ni zao la kwanza la ubia
kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick, ambapo kutokana na makubaliano hayo
wilaya hiyo imeanza kupokea ushuru huo na fedha za kurudisha kwa jamii (CSR)
kwa kiwango kikubwa kuliko awali, huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri
hizo mbili kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika utaratibu ulio bora.
“Kupitia fedha hizi tayari miradi mbalimbali imeanza
kuibuliwa ikiwemo ujenzi wa jingo la wagonjwa wan je (OPD) na kliniki
zitakazogharimu Sh Bilioni 3.2 na miradi mingine ya maji, pia halmashauri ya
Kahama imeendelea kubuni miradi mbalimbali yenye tija kwa maendeleo ya vijana,
wenye ulemavu na wanawake.
“Kwa upande wa halmashauri ya Msalala tumekaa na vikundi
mbalimbali katika kata zinazozunguka migodi hii ambapo Sh Milioni 900 zimetengwa
kusaidia maendeleo ikiwemo ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike, kuimarisha kituo cha afya Bugarama, huduma za
maji na miradi mingine ya maendeleo itakayowagusa moja kwa moja wananchi,”
amesema Macha.
Akifafanua kuhusu malipo hayo, Meneja Mkuu wa Migodi ya
Bulyanhulu na Buzwagi, Benedict Busunzu amesema migodi ya Twiga Minerals chini ya Kampuni
ya Barrick Tanzania hulipa ushuru wa huduma kila baada ya miezi sita kwa
halmashauri ambazo migodi yao inaendesha shughuli zake kulingana na mapato yao
ya kila mwaka.
“Licha ya kulipa kodi stahiki bado tumekuwa
tukijishughulisha kuhakikisha migodi yetu inakuwa mdau muhimu wa maendeleo
kupitia sera yake ya maendeleo kwa jamii ili kuunda fursa endelevu za kiuchumi
na maendeleo kwa ujumla kwa jamii zinazozunguka migodi ya Barrick na kuinua
uchumi wa wilaya pamoja na kuboresha ustawi wa maisha ya wenyeji, lengo ni
kuona mamlaka husika zinaelekeza fedha hizi katika miradi inayolenga kuwaletea
wananchi maendeleo katika maeneo yanayotuzunguka,” alisema.
Katika hatua nyingine, Busunzu ameeleza kuwa wameendelea
kutekeleza sera ya maendeleo kwa jamii, ambapo kwa mwaka jana mgodi wa Buzwagi
ulitenga Sh Bilioni 2.3 kwa kuwekeza katika jamii kuboresha huduma mbalimbali,
huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono na kwamba kupitia uwepo
wao wananchi wataendelea kunufaika zaidi.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila amewahimiza viongozi wa halmashauri husika zilizopokea fedha hizo kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija kwa wananchi wa maeneo lengwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akizungumza baada ya kupokea hundi hizo.
Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu akizungumza baada ya kuzikabidhi halmashauri za Mji wa Kahama na Msalala hundi ya Sh Bilioni 1.5 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika jamii inayoizunguka migodi hiyo.
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Joachim Simbila
Viongozi wa Halmashauri ya Msalala wakifurahia baada ya kupokea hundi ya Sh Milioni 376, 004,787 kutoka mgodi wa Bulyanhulu
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba (katikati) wakipokea hundi ya Sh Bilioni 1,159,817,107 kutoka mgodi wa Buzwagi iliyokabadhiwa na Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu (kushoto)
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege (katikati) akipokea hundi ya Sh mMilioni 376,004,787 kutoka kwa Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Busunzu (kushoto) na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha