Jaquline Kisanga akizungumza baada ya kuchukua fomu
BAADA ya
Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Nyamagana
mkoani Mwanza kumuunga mkono kwa kumsindikiza kuchukua fomu ya kuwania ubunge wa jimbo hilo, Mwenyekiti wa
Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA) mkoa wa Mwanza, Jaquline Kisanga,
ametaja vipaumbele vyake, huku akiwahimiza wenzake kuacha uoga kugombea nafasi
za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti
huyo wa Bawacha Mwanza alisindikizwa na wanachama na viongozi wa Bawacha Nyamagana kuchukua fomu Julai 9, 2020 katika ofisi za Chadema Kanda ya Viktoria, ambapo baadhi ya wanawake
waliojitokeza kumsindikiza akiwemo Majona Zacharia ambaye ni
Katibu wa Baraza la Wanawake Isamilo na Veneranda Dioniz ambaye ni Katibu wa
BAWACHA kata ya Nyamagana, wamesema kuwa ifike wakati sasa wanawake waweze
kujisimamia na kuthubutu kugombea nafasi za uongozi huku wakiwatoa hofu
wanawake wengine.
“Viongozi wote watakaohitaji kuchukua
fomu wasisite kutuambia kama wanahitaji msaada wa wanawake, sisi tutaungana nao
kwa sababu sisi ni jeshi kubwa, na mimi kama kiongozi wao kwa Nyamagana niko
tayari kushirikiana na viongozi wote wanaohitaji msaada wetu,” amesema
Veneranda.
Kwa upande wake, Jaquline Kisanga baada
ya kuchukua fomu ya kuwania jimbo hilo, amesema chama chake kikimpa ridhaa
ataanza na miundombinu ya bararabara na changamoto za wanawake wanazokumbana
nazo wakati wa kujifungua.
“Endapo chama change kitanipa ridhaa ya
kukiwakilisha kwenye jimbo la Nyamagana, kwanza kabisa kipaumbele change
kitakuwa ni miundombinu kwa sababu akina mama ndiyo wanaoteseka zaidi na miundo
mbinu mibovu, pia kuhakikisha natatua changamoto zinazowakumba wakati wa
kujifungua.
“Tutawaondolea usumbufu wanaoupata wakati wa
kujifungua ikiwemo kutakiwa kwenda na vifaa vya kujifungulia wakati wengine
hawana uwezo wa kununua,pia miundombinu ya barabara nyingi za nyamagana ni
mibovu nitaanza kuirekebisha ili iweze kupitika kwa urahisi na isilete usumbufu
hasa nyakati za mvua,” amesema.
Jaquline akitoka katika ofisi za chama chake kuchukua fomu
Baadhi ya wanachama waliojitokeza kumsindikiza Jaquline Kisanga kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Nyamagana
Wanachama wakimpongeza baada ya kuchukua fomu