Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli
Na Damian Masyenene – Shinyanga Press
Club Blog
LEO Julai 16, 2020 Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amewaapisha viongozi wapya wakiwemo
wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala aliowateua jana
(Jumatano), ambapo amewasisitiza kuridhika na vyeo vyao, kuwa wavumilivu na
kwenda kutatua kero za wananchi katika maeneo yao ya kazi.
Hafla hiyo ya kuwaapisha viongozi
hao imefanyika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma ikihudhuriwa pia na Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na wakuu
mbalimbali wa mikoa na vyombo vya usalama.
Moja ya nukuu alizozitoa leo Rais
Magufuli ni ‘Katika kazi hizi kuridhika ni kitu muhimu sana’, ambapo aliwatolea
mfano viongozi mbalimbali wapya aliowaapisha leo ambao wamekuwa wavumilivu na
wariridhika na nyadhifa zao, akiwemo Mkuu mpya wa Wilaya ya Kongwa mkoani
Dodoma, Dkt. Seleman Serera ambaye ana Shahada udhamivu (PhD) na alikuwa
anapokea mshahara wa Sh 500,000 akaridhika na sasa amepanda cheo.
“Najaribu kutoa mifano hii ili wanaotusikiliza watuelewe,
nendeni mkafanye kazi katika maeneo yenu mkavumilie. Huko mnakokwenda mnakwenda
kutekeleza ilani ya CCM kwahiyo kila mmoja katika eneo lake akafanye kila
anachoona kinafaa kwa manufaa ya nchi na kuwaletea maendeleo wananchi wa eneo
husika.
.
“Tukazingatie maadili, tukachape kazi, msiende kuchukua muda
mrefu wa kujifunza ama kuzoea kazi….mkurugenzi wa TIC kahakikishe tunapata
wawekezaji wengi, tusiwazungushe wawekezaji, tunahitaji wawekezaji, kwahiyo
nikuombe Dokta kahakikishie mwenyekezaji anayekuja leo anapata fursa,” amesema.
Pia Rais Magufuli amewapongeza wale wote waliojitokeza
kuwania nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo amewaomba
kukazingatia nidhamu na maadili ya chama hicho.
“Niwathibitishie tu
kwamba hakuna mtu yeyote aliyetumwa na mimi, waziri mkuu, makamu wa rais, kama
kuna watu wanazungumza kwamba mimi nimewatuma ni uongo.
“Sababu naskia wanasema
eti wametumwa na Rais, sasa kama nimekutuma kwanini nihangaike kukutuma, si
ningesubiri tu kwenye uteuzi wa viti 10 nikakuteua,” amesema.