Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameonyesha kushangazwa na kitendo cha Taasisi
ya ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutaka kujenga ofisi nyingine wilayani Chato wakati tayari kulikuwa
na ofisi alizoikabidhi taasisi hiyo.
Kitendo hicho kimemlazimu Rais Magufuli kusema kuwa yeye siyo
mbinafsi kwani kitendo hicho kingetafsiriwa kwamba anapapendelea Chato ambako
ni nyumbani kwao.
Na badala yake amependekeza fungu lililotengwa kwa ajili ya
ujenzi wa ofisi ya Chato zipelekwe Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ambako hakuna
ofisi ya Takukuru.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Julai 22, 2020 wakati wa hafla ya uzinduzi
wa ofisi za Takukuru Wilaya ya Chamwino lenye thamani ya Sh Milioni 43.
Mbali na hayo, Rais Magufuli ameipongeza taasisi hiyo kwa
kazi kubwa iliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitano.
"Nashangaa mnaniambia mnataka kujenga ofisi Chato wakati tayari kuna ofisi ya ghorofa na iko mlimani niliwakabidhi, mimi siyo mbinafsi msijenge ofisi mbili mbili Chato," amesema.