KAYA ZILIZOJIKWAMUA NA UMASKINI AWAMU ILIYOPITA KUONDOLEWA KWENYE TASAF III AWAMU YA PILI



Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Tasaf kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga.

Na Marco Maduhu - Shinyanga

Walengwa wa mfuko wa maendeleo ya jamii wa kunusuru Kaya maskini Tasaf ambao wameondokana na umaskini katika awamu iliyopita, wanatarajiwa kuondolewa kwenye mpango huo, ili kuingizwa Kaya mpya ambazo zitanufaika na Tasaf 111 awamu ya pili.

Hayo yalibainishwa jana na kaimu mkurugenzi wa Tasaf kutoka makao makuu Fariji Mishael, wakati wakitambulisha rasmi zoezi la kuanza kufanya tathimini ya kubaini Kaya maskini, ambazo zilikuwa wanufaika wa Tasaf awamu iliyopita, na sasa siyo maskini tena ili waondolewe kwenye mpango huo.

Amesema mpango huo wa kunusuru Kaya maskini Tasaf III awamu ya pili, wanatarajia kuingiza majina ya walengwa wapya ili kuwainua kiuchumi, na kuziondoa zile Kaya ambazo zimeshaondokana na umaskini, lengo likiwa ni kuondoa umaskini kabisa hapa nchini.

“Zoezi hili la kufanya uhakiki kubaini kaya ambazo zilikuwa kwenye mpango wa Tasaf awali, na sasa siyo maskini tena litafanyika kwa muda wa wiki moja hapa Shinyanga na kuziondoa kabisa kwenye mpango huu, ili tuingize Kaya mpya ambazo ni maskini,” amesema Mishael.

“Baada ya uchaguzi mkuu kuisha ndipo zoezi rasmi la kuzibaini Kaya mpya ambazo ni maskini litaanza, ambapo litatanguliwa kwanza na Semina elekezi kwa watendaji ambao watafanya zoezi hili pamoja na kula kiapo, ili walifanye kwa usahihi na kutoingiza Kaya ambazo hazina sifa kama awamu zilizopita,” ameongeza.

Aidha amesema kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya taifa ya takwimu Tanzania (NBS) (2017-18) asilimia 60 ya walengwa wa Tasaf siyo maskini tena, huku tathimini ya mpango kwa walengwa wenyewe kiwango cha umaskini kimepungua kwa asilimia 10 hadi 12.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amewataka walengwa wa Tasaf ambao wataingizwa kwenye mpango huo, wazitumie fedha hizo kujikwamua kiuchumi, na siyo kuzitumia vibaya ikiwamo kuzinywea Pombe.

Pia amewataka maofisa wa Tasaf kwa kushirikiana na maofisa ugani na maendeleo, kutoa elimu kwa walengwa namna ya kutumia fedha hizo kwa usahihi kuwa kwamua kiuchumi, ikiwamo kufuga mifugo, kilimo, pamoja na kuibua miradi mbalimbali ambayo itawatoa kwenye umaskini.

Kaimu mkurugenzi wa Tasaf kutoka makao makuu Fariji Mishael, akielezea namna mpango wa Tasaf III awamu ya pili utakavyotekelezwa hapa nchini ikiwamo kuondoa Kaya ambazo zimeondokana na umaskini.

Kaimu mkurugenzi wa Tasaf kutoka makao makuu Fariji Mishael, akielezea namna mpango wa Tasaf III awamu ya pili utakavyotekelezwa hapa nchini ikiwamo kuondoa Kaya ambazo zimeondokana na umaskini.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye zoezi la kutambulishwa mpango wa Tasaf.



Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha Tasaf kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga.

Picha zote na Marco Maduhu
















Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464