KITUO CHA UBUNIFU MABUGHAI KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akisikiliza maelezo kuhusu kituo cha ubunifu kilichopo Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai kutoka kwa Mkufunzi na Msimamizi wa Kituo hicho Clara Mwinami wakati alipotembelea Chuo hicho kujionea shughuli za mbalimbali zinazofanywa.

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Viwanda na Biashara inakusudia kuwekeza katika kituo cha ubunifu kilichopo katika Chuo cha  Maendeleo ya Jamii Mabughai, Mkoa wa Tanga ili kukiwezesha kutoa elimu yenye tija kwa wahitimu na jamii kwa ujumla

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai kujionea shughuli za mbalimbali zinazofanywa na Chuo hicho.

Katibu Mkuu Dkt. John Jingu amesema kuwa amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe ili kukiwezesha Chuo cha Mabughai kutoa mafunzo ya ubunifu endelevu kwa jamii.

Amesema Mpango wa maboresho ya miundombinu na teknolojia ya Chuo hicho utashirikisha Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Chuo cha Mabhughai kilichoko chini ya Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.

"Teknolojia imebadilika sana mimi na Profesha Shemdoe tumekubaliana kufanya maboresho katika Chuo hiki tuone namna ya kukiwezesha kuwanoa wabunifu ili elimu inayotolewa iweze kuwa na tija kwa walengwa wetu ambao ni wanachuo na wananchi wa maeneo jirani" alisema Dkt. Jingu.

Aidha,  amesisitiza kuwa  Serikali inalenga kuwawezesha Wanafunzi kuwa na uwezo wa kujiajiri kupitia maarifa wanayopata na kuanzisha mtandao wa ajira kwa wahitimu ambao watafanya kazi kwa vitendo na hivyo kutengeneza fursa zaidi za mafunzo kwa wengine.

Katibu Mkuu Jingu amesema mpango wa maboresho kwa Chuo cha Mabughai utaanza hivi karibuni baada ya kukamilisha taratibu za maandalizi kwa ushirikiano wa SIDO na ni hatua mojawapo ya kushiriki katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda.

“Tumeshuhudia jitihada za Serikali zilivyotuwezesha kuingia katika Uchumi wa Kati miaka mitano kabla ya muda uliotarajiwa,wakati tukiendelea kujivunia hatua hii muhimu kushiriki kwa vitendo katika mabadiliko ya teknolojia” alisema.

“Kuna baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, Mfano kuna mbunifu ametoa ajira kwa watu zaidi ya 100, hii ni hatua mojawapo ya mafsnikio. Tunataka kukiwezesha Chuo hiki cha Mabughai kutengeneza wabunifu zaidi” alisema.

Amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Viawanda na Biashara inakusudia kuwawezesha vijana kupata ajira zitakazotokana na ubunifu kwa wahitimu na pamoja na wakazi wa maeneo jirani na Chuo.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya - Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii iko katika hatua za mwisho kuanzisha Kampuni ya ulinzi itakayomilikiwa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai ili kuwapa nafasi kuwapa nafasi wahitimu kujiajiri wanapotoka chuoni hapo.

“Tunataka kuanzisha kampuni ya chuo ambayo itakuwa inamilikiwa na chuo kama ilivyo SUMA JKT ili kuwapa fursa zaidi za ajira kwa vijana” alisema

Akiwa chuoni hapo Dkt. Jingu ameweza kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kituo cha ubunifu cha kidijitali kinacholenga kuwasaidia wanafunzi hao kubuni na kuendeleza maarifa wanayopata chuoni hapo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464