CHAMA cha ACT Wazalendo kimetangaza kuongeza muda wa uchukuaji fomu
za kugombea nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani hadi Julai 20
badala ya Julai 13 ya awali.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa hatua ya Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC) kufuta na kuanzisha majimbo mapya ya uchaguzi.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif
Sharif Hamad wakati wa ziara yake aliyoifanya ya kuhakiki uhai wa chama
Shangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Uamuzi huo umetokana na hatua ya kukatwa kwa baadhi ya majimbo na mengine kuongezwa,” alisema Maalim Seif.
Alisema hali hiyo imesababisha uchukuaji wa fomu za kugombea uongezwe
ili kuwapa muda wale ambao majimbo yao yameathirika na mengine
yamepunguzwa.
Maalim Seif alisema sasa kuna idadi ya majimbo 50 badala ya majimbo ya awali yaliyokuwa 54 kwa Unguja na Pemba.
“Hatua hiyo ya kuongeza muda itawapa nafasi wagombea kujipanga
katika safu za kugombea katika majimbo yao,” alisema Maalim Seif.
Hata hivyo ameitaka ZEC na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kufanya
uchaguzi wa huru na wa haki ili kila mmoja aweze kuridhika na
uendeshwaji wa uchaguzi huo.
Maalim Seif alisema chama chake kimejizatiti na kiko tayari kwa
uchaguzi, wanachosubiri ni tume itoe tamko la tarehe ya uchaguzi.
“Siku yeyote itakayotangazwa tupo tayari, tumejizatiti kwa uchaguzi,” alisema Maalim Seif.
Aidha Maalim Seif aliendeleza msisitizo wake wa kukemea rushwa na
kudai kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na agizo hilo basi amejiondoa
mwenyewe.
“Hatupo tayari kuona mtu anaingia katika uongozi kwa kupitia njia ya
rushwa, hatutolifumbia macho suala hilo,” alisema Maalim seif.
Aidha aliwataka wanawake kuchukua nafasi za kugombea katika majimbo ili kuongeza uwakilishi wao katika vyombo vya uamuzi.
Awali Katibu wa Habari na Uenezi wa ACT Wazalendo, Salim Bimani,
alivitaka vyama vingine vya upinzani kuzungumzia matatizo ya wananchi na
kuacha hujuma dhidi ya chama chao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464